Masumbwi

Cheka kurejea ulingoni Juni

DAR ES SALAAM: BONDIA Cosmas Cheka ametangaza kurejea tena ulingoni, akisema amerudi kwa dhamira ya kuwafundisha watu namna bora ya kucheza mchezo wa ngumi.

Akizungumza kwa kujiamini na SpotiLeo Cheka amesema kurejea kwake si tu kwa ajili ya mashindano, bali pia kushirikisha uzoefu wake kwa chipukizi wanaotaka kufanikiwa katika mchezo huo.

“Nimerudi tena, nimekuja kuwafundisha watu ngumi zinavyochezwa. Kikubwa ni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hapa nilipofika, watu wanapenda ngumi nawashukuru sana,” amesema Cheka.

Bondia huyo ameongeza kuwa mapenzi ya mashabiki yamekuwa chachu kubwa ya kumrudisha ulingoni, huku akiahidi kutoa burudani na mafunzo yatakayoinua kiwango cha mchezo wa ndondi nchini.

Cheka ni mdogo wa bingwa wa zamani wa ngumi za kulipwa Francis Cheka ambaye amekuwa na rekodi nzuri kimataifa.

Rekodi yake aliwahi kushinda ubingwa wa WBO Pasific nchini Thailand. Amecheza jumla ya mapambano 58 ya ndani na nje ya nchi na kati ya hayo, ameshinda 29, amepoteza 21 na kupata sare nane.

 

Related Articles

Back to top button