Mfaume Mfaume atoka Hospitali

DAR ES SALAAM: BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Mfaume Mfaume ameruhusiwa kutoka hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dar Es Salaam Amana, baada ya kupata ajali ya bodaboda maeneo ya Tabata jijini humo.
Mfaume anayetoka gym ya Naccoz anayesimamiwa na Paf Promotion, amepata ajali hiyo jana usiku na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Amana kwa matibabu zaidi akiwa na shabiki yake Cheduo anayetajwa kuvunjika mkono.
Akizungumza na Spotileo, Mkurugenzi wa Paf Promotion, inayomsimamia bondia huyo, Fadhili Maogola amesema Mfaume amepata ajali hiyo jana saa mbili usiku alipokuwa anatoka kwenye kikao cha kazi katika eneo la Buguruni. Kikao ambacho kilikuwa na viongozi wa menejimenti inayomsimamia kwenye kazi akiwa na shabiki wake Peter Mubarak ‘Cheduo ambaye alikuwa dereva wa pikipiki waliopata nayo ajali.
“Hali ya majeruhi hao inaendelea vizuri, Mfaume ametolewa hospital leo baada ya kupata matibabu ya majeraha aliyoyapata katika ajali hiyo, ameruhusiwa na yupo nyumbani,” amesema Mkurugenzi huyo.
Amewashusha presha ya mashabiki wa Mfaume na kuweka wazi kuwa bondia huyo hajapata majeraha makubwa wala hajavunjika zaidi ya kupata majeraha madogo madogo.