Yanga Muembe Makumbi City hapatoshi
ZANZIBAR: MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, wanatarajia kushuka dimbani leo saa 1:00 usiku kuikabili timu ya Muembe Makumbi City FC katika mchezo wa Kombe la Muungano utakaochezwa visiwani Zanzibar.
Muembe Makumbi City, inayoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar, kwa sasa inashika nafasi ya nane kwenye msimamo ikiwa na pointi 33 baada ya michezo 22. Licha ya nafasi hiyo, timu hiyo haiwezi kubezwa, hasa ikizingatiwa kwamba mara nyingi timu ndogo huongeza nguvu na ari zinapokutana na vigogo, wakitambua ni jukwaa la kujitangaza.
Kwa upande wa Yanga, wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na pointi 47 katika michezo 22. Kikosi hicho kinaonekana kuwa imara zaidi msimu huu, kikijivunia safu kali ya ushambuliaji iliyofunga mabao 44 huku ikiwa na ulinzi bora ulioruhusu mabao matatu pekee.
Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Conclaves , amesema wamejiandaa vyema kwa ajili ya mchezo huo na hawataubeza, licha ya tofauti ya viwango vya ligi.
“Kwetu sisi ni furaha kuwepo Zanzibar, tunajisikia kama tuko nyumbani. Tumekuwa na kumbukumbu nzuri hapa. Kombe la Muungano ni sehemu muhimu ya kuimarisha umoja. Tutawapa nafasi wachezaji wote lakini lengo ni kuendelea kuonesha kiwango chetu na kushinda mechi zote ikiwezekana kutwaa ubingwa,” amesema kocha huyo.
Kwa upande wa Muembe Makumbi City, nahodha wake, Yakoub Said, amesema wamejipanga kuhakikisha wanatoa upinzani mkali dhidi ya Yanga.
“Tunajiandaa vizuri kuhakikisha tunafanya vizuri. Tutacheza kama mechi nyingine yoyote lakini tukiwa na ari ya kuonesha uwezo wetu. Tunaamini tuna nafasi ya kupambana na kushinda,” amesema.




