Simeone awapa tano wachezaji wake

MADRID, Hispania: KOCHA wa Atletico Madrid, Diego Simeone, ameisifu timu yake kwa kuonesha moyo wa kupambana na kufanikiwa kulinda matokeo muhimu yaliyoipeleka klabu hiyo hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya
Simeone Amesema wachezaji wake walionesha nidhamu na kujituma mbele ya mashabiki wao, jambo lililochangia mafanikio hayo makubwa ambapo Atletico sasa wanasubiri kumenyana na Arsenal.
Kwa upande wa FC Barcelona, kocha Hansi Flick amesema licha ya timu yake kupambana kwa nguvu, walikosa bahati ya kusonga mbele.
Aliwapongeza wachezaji wake kwa ari waliyoionesha lakini akakiri bado kuna maeneo yanahitaji maboresho ili kuwa bora zaidi.
Katika mchezo huo wa marudiano uliochezwa Madrid, Barcelona walianza kwa kasi wakisawazisha matokeo ya jumla kupitia mabao ya Lamine Yamal dakika ya nne na Ferran Torres dakika ya 24. Hata hivyo, Atletico Madrid walijibu mapema dakika ya 31 kupitia bao la Ademola Lookman lililowarejesha kwenye uongozi wa jumla.

Kipindi cha pili kilishuhudia Barcelona wakitawala umiliki wa mpira wakiongozwa na Pedri na Gavi, lakini walishindwa kupata bao la ziada. Mchezo uligeuka kuwa mgumu zaidi kwao baada ya Eric Garcia kutolewa kwa kadi nyekundu kufuatia kuzuia nafasi ya wazi ya kufunga, uamuzi uliothibitishwa na VAR.
Licha ya kufungwa mabao 2-1 katika mchezo huo, Atletico walitinga nusu fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2, wakisubiri sasa mpinzani wao kati ya Arsenal na Sporting CP.




