Ligi Kuu

Simba, Fountain Gate vitani leo

ARUSHA. TIMU ya Simba SC leo inatarajiwa kushuka dimbani kuvaana na Fountain Gate FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na morali nzuri baada ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB.

Kocha Mkuu wa Simba, Steven Barker amesema kikosi chake kitacheza kwa mbinu tofauti na mchezo uliopita ili kuhakikisha wanapata ushindi muhimu.

“Maandalizi yetu ni mazuri, na tumejipanga kucheza tofauti kimbinu ili kufikia malengo yetu ya kushinda,” amesema Barker.

Kwa upande wa Fountain Gate FC, Kocha Mkuu Abubakar Ally amekiri kuwa mchezo huo ni mgumu kutokana na ubora wa wapinzani wao, lakini wamejipanga kupambana.

“Ni mechi ngumu, tunakutana na timu nzuri yenye wachezaji bora. Kiufundi ni mchezo tofauti kabisa, na tayari nimezungumza na wachezaji wangu kuhusu nini cha kufanya,” amesema.

Kwa mujibu wa msimamo wa ligi, Simba SC inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 36 baada ya michezo 17, ikiwafuatia vinara Yanga wenye pointi 44 katika michezo 18.

Kwa upande wa Fountain Gate FC, hali si shwari kwani ipo nafasi ya 14 ikiwa na pointi 16 baada ya michezo 18, hivyo italazimika kupambana kwa nguvu zote kujinasua kutoka kwenye hatari ya kushuka daraja.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na tofauti ya malengo ya timu hizo, Simba ikisaka kuendelea kuwania ubingwa huku Fountain Gate ikihitaji pointi muhimu kujinasua mkiani mwa msimamo.

 

Related Articles

Back to top button