Zawadi Kutaka kukiwasha leo Scoatland

GLASGOW: MATUMAINI ya Tanzania katika mashindano ya Michezo ya Jumuiya ya Madola 2026 yataelekezwa kwa bondia Zawadi Kutaka, anayetarajiwa kupanda ulingoni leo kuwania nafasi ya kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano yanayoendelea Glasgow, Scotland.
Zawadi atashuka dimbani kumenyana na Rapelang Maselela wa Lesotho katika pambano la robo fainali la uzani wa kilo 57 kwa wanawake, huku ushindi ukimhakikishia tiketi ya kucheza nusu fainali.
Pambano hilo litafanyika katika ukumbi wa SEC Hall 5 na limepangwa kuanza saa 12:45 jioni kwa saa za Scotland, sawa na saa 2:45 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, likiwa pambano la 135 kwenye ratiba ya mashindano.
Kwa mujibu wa ratiba ya mashindano, ushindi katika hatua hiyo utamuweka Zawadi hatua moja tu kutoka kupigania medali, jambo litakalokuwa mafanikio makubwa kwa Tanzania kwenye michezo hiyo.
Tanzania inaendelea kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola 2026 ikiwa na lengo la kufanya vizuri katika michezo mbalimbali, huku macho ya Watanzania yakielekezwa kwa wawakilishi wake wanaowania heshima ya taifa.




