Msigwa: Afcon ni jukumu letu sote Watanzania

DAR ES SALAAM: SERIKALI imewataka Watanzania kuchukua umiliki wa pamoja wa mashindano ya Africa Cup of Nations 2027 (AFCON 2027), ikisisitiza kuwa mashindano hayo ni fursa ya kitaifa ambayo manufaa yake hayatabaki serikalini pekee, bali yataenea kwa wananchi na sekta mbalimbali nchini.
Akizungumza wakati wa kikao cha wadau kujadili maandalizi ya fainali hizo zitakazofanyika mwaka ujao nchini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema AFCON ni tukio la kitaifa ambalo linapaswa kumilikiwa na kila Mtanzania.
Msigwa amesema mafanikio ya mashindano hayo hayatakuwa ya serikali pekee, bali yatagusa wananchi wote kupitia fursa za kiuchumi na kijamii.
“Tunatoa wito kwa Watanzania wote kuichukulia AFCON kama tukio la kitaifa, si la serikali pekee. Faida na neema zitakazotokana na mashindano haya ni za Watanzania wote,” amesema.
Ametaja baadhi ya maeneo yatakayoguswa moja kwa moja kuwa ni miundombinu, huduma za malazi, usafiri, biashara ndogo ndogo na huduma za ukarimu, hivyo wananchi wanapaswa kujipanga ili kunufaika na fursa hizo.
Aidha, Msigwa amesema serikali imefungua milango kwa wananchi, taasisi na wadau mbalimbali kutoa mawazo, mapendekezo na ushauri utakaosaidia kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa mafanikio.
Amesema ushiriki wa wananchi ni muhimu katika kufanikisha mashindano hayo na kwamba Watanzania wanapaswa kuachana na malalamiko na badala yake kuleta suluhisho na mawazo yenye tija.
Msigwa aliongeza kuwa mafanikio ya AFCON yataakisi taswira ya nchi nzima kimataifa, hivyo kila Mtanzania ana jukumu la kuhakikisha mashindano hayo yanaacha urithi chanya kwa taifa.




