Africa

Serengeti girls ya motooo!

MONASTIR: TIMU ya soka ya Taifa ya Wanawake chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Girls), imeanza vyema kambi yake ya mazoezi kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tunisia kwenye Uwanja wa Mustapha Ben Jannet Monastir nchini Tunisia jana.

Serengeti Girls imeweka kambi mjini Monastir nchini Tunisia kwa ajili ya maandalizi ya mechi za kufuzu fainali za kombe la dunia zilizopangwa kufanyika Morocco baadae mwaka huu.

Timu hiyo iliyo chini ya kocha Bakari Shime ilitawala vipindi vyote vya mchezo na kufunga bao moja katika kipindi cha kwanza na mawili katika kipindi cha pili.

Yasinta Michael ndiye aliyeanza kufungua mlango wa ushindi kwa kufunga bao la kuongoza dakika ya 17 kabla Bahati Steven hajaongeza bao la pili dakika ya 53 na Aalya Juma kufunga bao la tatu katika dakika ya 90.

Akizungumza baada ya mechi hiyo Kocha Shime alisema amefurahia mchezo mzuri uliooneshwa na wachezaji wake.

“Nimeridhishwa na nilichokitaka wachezaji wamefanya vizuri na matumaini yangu mechi ijayo tutafanya vizuri zaidi,” amesema.

Serengeti inatarajiwa kucheza mechi ya marudiano na wapinzani wao hao Aprili 4 kabla ya kuelekea Gaborone siku inayofuata kucheza na timu ya Taifa ya Botswana katika mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia.

Endapo itaiondoa Botswana, itacheza na Afrika Kusini hatua inayofuata.

Timu hiyo imeshawahi kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022 zilipofanyika India na kuweka historia kwa soka la wanawake kufuzu kombe la dunia.

Related Articles

Back to top button