Africa

MICHUANO YA KLABU AFRIKA: Wawakilishi wa Tanzania waanza na mteremko

WAWAKILISHI wa Tanzania, Yanga na Simba kwenye Ligi ya Mabingwa na Singida Fountain
Gate na Azam kwenye Kombe la Shirikisho Afrika wapo kwenye hekaheka za kutupa karata zao za kwanza katika hatua ya awali kwenye michuano ya Caf msimu wa 2023/24.

Timu za Tanzania zinaonekana kama zimeanza na timu mchekea au mteremko katika mechi zao hizo za kwanza na hivyo zina nafasi kubwa ya kucheza hatua ya makundi kama
zitagangamala.

Vigogo hao wa soka la Tanzania, Yanga wataanzia ugenini watakapoenda kuwakabili Association Sportive d’Ali Sabieh ya nchini Djibouti.

Mtanange wa kwanza utachezwa kati ya Agosti 18 na 20 kwenye Uwanja wa El Hadj Hassan Gouled Aptidon, huku michezo ya marejeano ikipigwa kati ya Agosti 25 na 27 kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Yanga wanashuka kwenye mchezo huo ikiwa mara yao ya kwanza kucheza dhidi ya wababe hao wa zamani wa Ligi Kuu ya Djibouti.

Wakati Simba wao wataanza kutupa karata yao kwenye raundi ya kwanza wakisubiri mshindi kati ya Power Dynamos ya Zambia dhidi ya African Stars ya Namibia. Kwenye Kombe la Shirikisho Tanzania itawakilishwa na Azam na Singida Fountain Gate FC.

Makocha wa timu zote nne; Yanga inayonolewa na Miguel Gamondi, Simba Roberto
Oliveira, Azam Youssoupha Dabo na Hans van der Pluijm wa Singida Fountain Gate hivi sasa watakuwa wanaumiza kichwa kwa kufanyia kazi mbinu ambazo zitawaletea matokeo chanya kwenye michezo hiyo ambayo huchezwa kwa hesabu kubwa ndani na nje ya uwanja.

Kulingana na ubora na udhaifu wao kwenye michezo yao ya hivi karibuni, hawa ndio  wapinzani wa Simba, Yanga Ligi ya Mabingwa na Singida Fountain Gate na Azam kwenye Kombe la Shirikisho barani Afrika.

WAPINZANI WA YANGA
Mabingwa mara nyingi zaidi wa ligi ya Djibouti wanaofahamika kama Association Sportive d’Ali Sabieh/Djibouti Telecom, AS Ali Sabieh au ASAS Djibouti Telecom, watakuwa na kibarua kizito cha kupepetana na mabingwa wa Tanzania katika hatua ya awali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika wakianzia nyumbani Djibouti na kumalizia
Dar es Salaam.

Kwa msimu huu katika ligi inayoendelea wapo nafasi ya pili na alama 37 nyuma ya vinara
wa ligi hiyo, CF Garde Republicaine/ SIAF yenye alama 39. Uwezekano wa Asas kutwaa
ubingwa utategemea matokeo ya mechi mbili za mwisho katika ligi yao.

Beki wa zamani wa Simba, Gilbert Kaze ndiye mchezaji pekee katika kikosi hicho
aliyewahi kucheza Tanzania.

Kikosini wana wachezaji watano wa kigeni watatu wakitokea nchini Burundi, mmoja Togo na mwingine Nigeria. Gilbert Kaze – Burundi, Sudi Ntirwaza – Burundi, Haruna Manirakiza-Burundi, Fatai Odutula -Nigeria, Kokuo Djamessi-Togo.

Kati ya mara saba walizotwaa ubingwa wa Djibouti, mara sita ni mfululizo wakitwaa ubingwa huo kuanzia msimu wa 2012/13 mpaka 2017/18 wakati taji jingine moja wakilitwaa 2008.

Mechi zao zinapigwa katika dimba la El Hadj Hassan Gouled Aptidon katika mji mkuu wa
nchi hiyo, Djibouti City.

Ligi ya Djibouti si ligi maarufu barani Afrika ila ushindani umeongezeka baada wawekezaji kadhaa kuwekeza kwenye baadhi ya klabu katika ligi hiyo ikiwemo AS Arta/Solar 7 iliyofanikiwa kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo 2020/2021 na 2021/22 wakiwa na wachezaji wakubwa kama Solomon Kalou na Alex Song.

Iwapo itapenya kwenye hatua ya kwanza, Yanga inatarajiwa kuwakabili kati ya Al Merrikh ya Sudan au AS Otoho ya Congo Braz- zaville. Al Merrikh, wao wana rekodi nzuri kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa ambapo msimu uliopita waliishia hatua ya makundi.

Hata hivyo, Merrikh wanaonekana kuwa washindani wagumu zaidi ikichagizwa na kila mara kucheza hatua ya makundi kama ilivyo Al Hilal ambayo iliiondosha Yanga kwenye hatua ya kwanza msimu wa 2022/23.

Wakati wapinzani wao AS Otoho ya Congo Brazzaville tangu waanze kushiriki michuano hiyo miaka mitano sasa hawajawahi kufuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa. Hatua kubwa waliyopiga ni kucheza makundi mara mbili upande wa Shirikisho, ikitokea wamemtupa nje Merrikh, watavaana na kati ya Yanga au Asas Djibouti.

WAPINZANI WA SIMBA
Simba huenda ikawakabili Power Dynamos ya Zambia au African Stars ya Namibia ambapo timu zote hazina rekodi nzuri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa. Mabingwa hawa wa Ligi Kuu ya Zambia watakuwa wakisaka rekodi yao mpya kwenye Ligi ya Mabingwa baada ya kuwa na rekodi mbovu kwenye michuano hii.

Power Dynamos wao wamecheza Ligi ya Mabingwa Afrika mara tatu mwaka 1998, 2001 na
mara yao ya mwisho kushiriki michuano hiyo ilikuwa 2012 walipoishia raundi ya pili.

Wakati Africa Stars ambayo ilianzishwa mwaka 1961 hawana rekodi nzuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika katika kipindi cha miaka 61 wamefanikiwa kucheza mara mbili michuano hii mikubwa mwaka 2019 walipoishia raundi ya kwanza na 2020 walipoishia hatua ya awali.

Moja kati ya wawili hawa atakayefuzu anaenda kukutana na Simba ambayo itaanzia hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na kuwapo kwenye timu 10 bora barani Afrika.

WAPINZANI WA AZAM
Bahir Dar Kenema, iliyoanzishwa mwaka 1971 ni miongoni mwa timu kongwe nchini
Ethiopia wapinzani hawa wa Azam hii ni mara yao ya kwanza kushiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Azam wanarudi kujiuliza msimu wa 2023/24, baada ya msimu uliopita kuondolewa kwenye raundi ya pili dhidi ya Al Akhdar ya Libya.

Kenema wamepata nafasi hii baada ya msimu uliopita kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Ethiopia na mshindi kati ya timu hizi anaenda kukutana na Club Africain ya Tunisia.

WAPINZANI WA SINGIDA
Hii ni vita ya ndugu wawili wakati Singida watakapokuwa wanawakabili timu ya Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) ya Zanzibar kwenye hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho barani
Afrika.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button