Mtibwa Sugar yahamishia hasira kwa Azam

DAR ES SAAAM: MTIBWA Sugar imesema hasira zao za kupoteza mchezo uliopita wanazihamishia katika mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Wakatamiwa hao wa Morogoro wametoka kupoteza dhidi ya Singida Black Stars mabao 3-1 mwishoni mwa wiki na sasa wana kibarua Kizito cha kusaka pointi tatu mbele ya matajiri wa Dar es Salaam Azam FC.
Kocha Mkuu Yusuph Chipo amesema wameingia uwanja wa mazoezi na kutathmini makosa yao kwa lengo la kurekebisha ambapo anaamini wanarudi na nguvu mpya kwenye uwanja wa mapambano.
Amesema kuwa ushindani wa Ligi Kuu msimu huu umeongezeka kwa kiasi kikubwa ambapo kila timu inapigania pointi, hali inayofanya kila mechi kuwa na presha kubwa.

“Ni ligi yenye ushindani mkubwa, lakini bado tunaamini katika ubora wa kikosi chetu. Tunachohitaji ni utulivu na kupunguza makosa ili kufanya vizuri dhidi ya Azam FC,” amesema Chipo.
Kocha huyo aliwataka mashabiki wa Mtibwa Sugar kuendelea kuwa nyuma ya timu hiyo akiahidi kuwa watarejea kwenye kiwango chao.
Wakati huo huo, Azam FC imeweka wazi dhamira ya kuendeleza wimbi la ushindi itakapokutana na Mtibwa Sugar, kufuatia ushindi wa mabao 2-0 walioupata dhidi ya KMC katika mchezo uliopita.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Msemaji wa Azam FC Hasheem Ibwe amesema wanaiheshimu Mtibwa Sugar kutokana na ubora wao wa kumiliki mpira na uwezo wa wachezaji wake mmoja mmoja.
“Tunatambua ubora wa Mtibwa, lakini sisi tupo kwenye morali nzuri baada ya ushindi uliopita na lengo letu ni kuendeleza matokeo chanya,” alisema Ibwe.




