Baraka The Prince amkataa Dudu Baya

DAR ES SALAAM: Msanii wa Bongo Fleva, Baraka The Prince, amezua mjadala mzito baada ya kutoa kauli kali kuhusu wasanii wawili wakubwa kutoka Mwanza, Farid Kubanda (FID Q) na Godfrey Tumaini (Dudu Baya), akieleza mtazamo wake kuhusu nani ana heshima na mamlaka ya kimuziki katika Jiji la Mwanza.
Akizungumza kupitia mahojiano na mitandao ya kijamii, Baraka The Prince amesema kuwa FID Q ndiye msanii anayeutawala Mkoa wa Mwanza kimuziki, huku akidai kuwa Dudu Baya anaishi nje ya jiji hilo, hivyo hana nafasi ya kudai hadhi ya “mtoto wa mjini” wa Mwanza.
“Wakina FID Q kwao ndiyo mjini. Dudu Baya kwao ni nje ya mji, vijijini kabisa. Hata asije akasema yeye ni mtu wa Mwanza mjini, aseme ni mtu wa nje kidogo,” amesema Baraka.
Kauli ya ‘Watoto wa Mjini’
Baraka The Prince ameendelea kusisitiza kuwa wasanii waliokulia katikati ya Jiji la Mwanza wana nafasi ya pekee katika kuwakilisha mji huo, akijitambulisha yeye na FID Q kama miongoni mwa “watoto wa mjini” wa Mwanza.
“Sisi ndiyo watoto wa mjini. Mimi kama mtoto wa Mwanza, ninaelewa uhalisia wa mjini,” ameongeza.
Mjadala Wazidi Kushika Kasi
Kauli hizo zimezua mjadala mpana miongoni mwa mashabiki wa hip hop na Bongo Fleva, wengi wakitofautiana juu ya vigezo vinavyopaswa kutumika kumpa msanii hadhi ya kuwakilisha mkoa au jiji fulani je, ni mahali alipozaliwa, alikokulia, au mchango wake katika muziki?
Wadau wa muziki wameeleza kuwa tofauti za kimtazamo kati ya wasanii ni sehemu ya ushindani wa kawaida wa kisanaa, huku wakisisitiza umuhimu wa kuheshimiana na kuacha muziki uongee zaidi kuliko kauli zenye utata.
Stori hii inaendelea kuvuta hisia za mashabiki, huku wengi wakisubiri kuona iwapo wasanii waliotajwa watajibu au kuchukua msimamo wao kuhusu kauli hiyo.




