Onesho la Burna Boy laondoa tofauti zake na Wakenya

NAIROBI: MWANAMUZIKI nyota wa Nigeria Burna Boy Jumamosi ya Machi 2, 2025 alikuwa katika Jiji la Nairobi nchini Kenya na alitumbuiza katika tamasha lililofanyika Bustani ya Uhuru.
Baadhi ya mashabiki waliofika katika tamasha hilo walifurahia saa mbili za mwanamuziki huyo jukwaani kwa namna alivyokuwa akijituma kucheza kwa bidii na kuimba kitendo kilichowasahaulisha Wakenya yote aliyowatendea miaka kadhaa iliyopita.
“Leo amekuwa mkubwa, nimekuja kwenye tamasha lake kwa sababu nilitumai Burna Boy aliyeshuka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) wakati huu hakuwa yule yule Burna Boy wa miaka ya 2014, 2017 na 2019 na kweli amecheza vizuri jukwaani na amenifurahisha ingawa bado kusahau alichotufanyia miaka hiyo ya nyuma,” alisema shabiki mmoja.
Shabiki huyo aliendelea kusema kwamba Burna Boy hana sifa nzuri na wakenya tangu alipokuwa huko kwa mara ya kwanza kurekodia Coke Studio Africa mwaka wa 2014 ambapo alizungumza mabaya kwa waandishi wa habari Pamoja na wakenya kwa ujumla.
Lakini, pengine, kumbukumbu kuu zaidi ambayo Burna aliweka katika akili za Wakenya wengi ni wakati alipopangiwa kutumbuiza katika klabu ya usiku ya Privee iliyokuwa ikivuma huko Westlands, Nairobi, Aprili 1, 2017 ambapo alipanda jukwaani usiku mnene na kutumbuiza kwa dakika chache tu kisha Kwenda zake kisha akawafungia kila mkenya aliyekuwa akiandika kitu kumsema katika ukurasa wake wa X.
Wakati mtangazaji mmoja wa redio mjini Nakuru aliposema kuwa hatacheza tena nyimbo zake kwenye kipindi chake, Burna Boy alimjibu akisema kwamba alikuwa na uwezo mkubwa wa kununua redio nzima anayofanyia kazi na kuigeuza kuwa kasha la kuwekea majivu na akaita Wakenya wote ‘wakulima’na aliahidi kama atarudi tena Kenya atawapima watakaohudhuria tamasha lake kwa sababu hataki Wakenya mabubu kwenye maonesho yake.
Lakini kwa namna alivyojituma katika onesho lake la jana imeonesha kwamba wakenya wamemsamehe kwa alichowafanyia kwa sababu wote walionekana wakiburudika naye katika kila alichoimba.