Geay: Nipo tayari kwa mbio za Daegu

DAR ES SALAAM: MWANARIADHA nyota wa Tanzania, Gabriel Geay, ameweka wazi kuwa yupo tayari kutetea heshima yake katika mbio za kimataifa za Daegu Marathon zitakazofanyika Jumapili ya wiki hii nchini Korea Kusini.
Geay alithibitisha kurejea huko katika mazungumzo na Spotileo akisema amejipanga vizuri kwenda kushindana na kutetea nafasi hiyo kwa mara nyingine.

Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Februari 22, mwaka huu, zikikusanya wanariadha bora wa dunia, huku Geay akiwa miongoni mwa majina makubwa yatakayokimbia baada ya kufanya vizuri mwaka jana.
Katika mbio hizo za Daegu ya mwaka jana, nyota huyo aliandika historia kwa kuibuka mshindi wa kwanza kwa muda wa saa 2:05:20 na kuipa Tanzania ushindi mkubwa katika mashindano hayo ya hadhi ya juu duniani.
Mwaka jana alimshinda shujaa wa Ethiopia aliyeshinda mbio za marathon Dubai mwaka juzi Addisu Gobena.



