Yanga Princess yamrejesha Oluwayemisi

DAR ES SALAAM- TIMU ya Yanga Princess imeendelea kuimarisha kikosi chake baada ya kutangaza rasmi kumrejesha mshambuliaji wake wa zamani, Oluwayemisi Samwel, raia wa Nigeria.
Mchezaji huyo anarejea ndani ya kikosi hicho baada ya msimu uliopita kuitumikia TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambako alipata uzoefu muhimu katika mashindano ya ngazi ya juu barani Afrika.
Hata hivyo, kurejea kwake hakutakuwa rahisi moja kwa moja kupata nafasi ya kudumu kikosini, kwani atakutana na ushindani mkali kutoka kwa Jean Mukandayisenga aliyetikisa nyavu mara 15 katika michezo 11 akitajwa kama mchezaji hatari kwa sasa Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu.
Ujio wa Oluwayemisi unatarajiwa kuongeza ushindani wa ndani na kuipa benchi la ufundi chaguo pana katika eneo la ushambuliaji, huku mashabiki wakisubiri kuona ni nani atajihakikishia namba ya kudumu kikosini.




