Mabadiliko makubwa yanakuja Simba – Ahmed

DAR ES SALAAM: MSEMAJI wa Simba, Ahmed Ally, amesema klabu hiyo imegeuza kipindi hiki cha mapumziko ya ligi kuwa fursa ya kufanya mabadiliko makubwa ndani ya kikosi, ikianzia na tathmini ya mechi zote walizocheza msimu huu hadi mchakato wa kupata benchi jipya la ufundi.
Akizungumzia kinachoendelea ndani ya klabu hiyo, Ahmed alisema ligi imesimama kupisha maandalizi ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), jambo lililowapa nafasi viongozi wa Simba kukaa chini na kupitia kwa kina mwenendo wa timu katika mashindano ya ndani na yale ya kimataifa.
Alisema tathmini hiyo ina lengo la kubaini maeneo yote yanayohitaji maboresho ili pindi dirisha la usajili litakapofunguliwa waende kufanya usajili sahihi utakaoongeza ushindani ndani ya kikosi.

Aidha, ametaja hatua nyingine muhimu kuwa ni mchakato unaoendelea wa kupitia maombi ya makocha mbalimbali waliojitokeza kuifundisha Simba, akibainisha kuwa uongozi uko makini kuhakikisha wanampata mwalimu bora atakayeliletea timu matokeo na kuinua viwango vya wachezaji.
“Kazi inaendelea vizuri. Tunapitia maombi ya makocha kwa umakini mkubwa. Tunataka kocha mzuri, atakayekuja kuinufaisha Simba na kuifanya timu iwe bora zaidi. Kufikia tarehe 28 Desemba, kikosi kitakaporejea mazoezini, tunatarajia benchi la ufundi litakuwa tayari,” alisema.
Ahmed aliwataka mashabiki wa Simba kuwa watulivu katika kipindi hiki cha mpito, akisisitiza kuwa mchakato wa maboresho unaendelea kwa utulivu na kwa maslahi ya klabu.




