68 Judo wapewa mbinu za kiufundi

WACHEZAJI na makocha 68 wamefundwa mbinu za kuwashinda maadui katika mafunzo ya wiki moja ya mchezo huo yaliyoandaliwa na Chama cha Judo Tanzania (JATA) chini ufadhili wa Ubalozi wa Ufaransa.
Akizungumza wakati wakifunga mafunzo hayo Dar es Salaam leo Rais wa JATA Zaidi Hamisi amesema mafunzo yalikuwa chini ya Mkufunzi kutoka Kituo cha Olimpiki Ufaransa Nicolas Malet.
“Tulitafuta namna ya kufanya kliniki ya Judo, tulijaribu kuwa na Ubalozi wa Ufaransa wakatuletea kocha kutoka kituo cha Olimpiki kule Ufaransa,
“Ubalozi wa Ufaransa kwa kushirikiana na Shirikisho la Judo la Ufaransa wametuletea Kocha kwa gharama zao, tunawashukuru kwa sapoti yao,”amesema.
Amesema kwa mafunzo waliyofundishwa anaamini wachezaji na walimu wamepata faida kubwa na anatgemea watapeleka kwenye klabu zao na wachezaji kuyatumia kujiimarisha na kupandisha viwango vyao.
Kwa upande wake, Nicolas amesema amekuwa akiwapa mbinu mbalimbali za kiufundi zinazotumika katika mashindano zitakazowasaidia kuwashinda wapinzani.
“Nawahimiza wachezaji kama wanataka kufanya vizuri wanatakiwa kufanya kazi, kuhakikisha kila siku wanajiwekea muda wa kufanya mazoezi ili kuwa bora na imara,”amesema.