Kwingineko

Wirtz amaliza ukame

FRNKFURT:KIUNGO wa Liverpool, Florian Wirtz, amemaliza ukame wake wa michango ya mabao baada ya kusaidia Liverpool kuichapa Eintracht Frankfurt 5-1 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa jana jumatano mjini Frankfurt.
Mchezaji huyo wa Ujerumani alitoa pasi mbili za mabao, akifanikisha ushindi mkubwa wa Liverpool baada ya kufungwa kwenye michezo minne mfululizo iliyopita. Wirtz, mwenye umri wa miaka 22, aliwasili Liverpool msimu huu wa kiangazi kwa pauni milioni 116 kutoka Bayer Leverkusen, na hadi jana mchango wake mzuri pekee ulikuwa kwenye Community Shield dhidi ya Crystal Palace.
Dhidi ya Frankfurt, Wirtz alimaliza ukame huo kwa kutoa asisti kwa Cody Gakpo na Dominik Szoboszlai, akionesha ni kwa nini Liverpool ilimtaka. Baada ya mchezo, Wirtz alikiri kuwa bado anaweza kufanya zaidi: “Nilijaribu kupata nafasi nzuri kipindi cha kwanza na kupoteza mpira na hapo hapo tukafungwa, lakini kipindi cha pili nilijaribu kuboresha nafasi zangu na kuonesha michango zaidi,” alisema.
Hiyo ni ishara kubwa kwamba Wirtz anaweza kuleta mabadiliko makubwa msimu huu, akisaidia kuimarisha kikosi cha Arne Slot na kuongeza nguvu kwenye eneo la wachezaji wa kati. Mashabiki sasa wanatarajia kuona kama ataendelea na kiwango hicho kikali.

Related Articles

Back to top button