Deschamps amsifu Mbappe kwa rekodi mpya kombe la dunia

EAST RUTHERFORD, Marekani: Kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps, amempongeza nahodha wake Kylian Mbappe baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Senegal kwenye mchezo wa ufunguzi wa Kundi I wa Kombe la Dunia 2026.
Mbappe aliiongoza Ufaransa kupata ushindi huo muhimu baada ya kufungua ukurasa wa mabao katika kipindi cha pili kabla ya kuongeza bao la tatu mwishoni mwa mchezo.
Bao lingine la Ufaransa lilifungwa na Bradley Barcola huku Ibrahim Mbaye akiifungia Senegal bao la kufutia machozi.
Mbali na kuisaidia timu yake kuanza mashindano kwa ushindi, mabao hayo mawili yamemfanya Mbappe kuwa mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ya Ufaransa akiwa amefikisha mabao 58 katika mechi 99 za kimataifa, akimpita Olivier Giroud aliyekuwa akishikilia rekodi hiyo.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Deschamps alisema Mbappe ni mchezaji wa kipekee ambaye mara nyingi amekuwa akikosolewa bila sababu za msingi licha ya mchango wake mkubwa ndani ya kikosi cha taifa.
“Bado wapo watu wanaomkosoa, lakini ukweli ni kwamba Mbappe ni mchezaji wa kipekee sana. Si kila kitu kinamwendea vizuri kila wakati, lakini ana uwezo wa kubadili matokeo ya mchezo kwa muda mfupi sana,” alisema Deschamps.
Kocha huyo aliongeza kuwa ana furaha kubwa kuona mshambuliaji huyo wa Real Madrid akivunja rekodi hiyo muhimu katika jukwaa kubwa la Kombe la Dunia, jambo ambalo linaongeza uzito wa mafanikio yake.
“Alishindwa kufunga katika michezo ya kirafiki kabla ya mashindano haya, lakini kuivunja rekodi hiyo kwenye Kombe la Dunia kunafanya mafanikio hayo kuwa makubwa zaidi,” alisema.
Licha ya ushindi huo, Deschamps alikiri kuwa timu yake ilikumbana na wakati mgumu katika kipindi cha kwanza ambapo Senegal ilionesha ushindani mkubwa na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga. Hata hivyo, Ufaransa ilibadilika kabisa baada ya mapumziko na kuonesha ubora wake wa kushambulia.
Kocha huyo alimpa sifa kiungo mshambuliaji Michael Olise wa Bayern Munich, ambaye alihamishwa kutoka winga kwenda eneo la kati katika kipindi cha pili, hatua aliyosema ilisaidia kuimarisha mchezo wa timu yake.
“Michael Olise alitupa kitu tofauti katikati ya uwanja. Uwezo wake wa kutunza mpira na kupiga pasi ulitusaidia kuwafikia washambuliaji kwa urahisi zaidi. Kadiri anavyogusa mpira mara nyingi, ndivyo tunavyokuwa bora zaidi,” alisema Deschamps.
Ufaransa, mabingwa wa dunia wa mwaka 1998 na 2018, sasa itaelekeza nguvu zake katika mchezo wake unaofuata dhidi ya Iraq utakaochezwa jijini Philadelphia Jumatatu ijayo, huku ikiwa na matumaini ya kuendeleza mwanzo wake mzuri wa mashindano.




