Simba, Yanga kupigwa Septemba 16

DAR ES SALAAM: SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza mchezo wa Ngao ya Jamii kufungua msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2025/26 utachezwa Septemba 16, 2025 Dar es Salaam.
Katika taarifa iliyoptolewa na TFF leo, imesema mchezo huo utawahuisisha bingwa wa Ligi Kuu Bara 2024/25 Yanga dhidi ya mshindi wa pili wa ligi Simba.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mfumo wa mashindano hayo hautahusisha tena timu nne kama ilivyokuwa msimu uliopita bali timu mbili tu kutokana marekebisho ya kanuni yaliyopitishwa katika kikao kilichopita cha Kamati ya Utendaji ya TFF.
“Moja ya marekebisho yaliyofanyika ni katika kanuni hiyo ambapo ikitokea mazingira kama ya sasa ambapo mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) yamebana ratiba za TFF, itachezwa mechi moja tu ya Ngao ya Jamii badala ya tatu ambapo huanzia na nusu fainali mbili na kumalizia na fainali,”ilisema.
Tanzania ni mwenyeji wa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN) zilizoanza Agosti 2, na zitamalizika Agosti 30 mwaka huu.
Pia, mwanzoni mwa Septemba timu ya Taifa (Taifa Stars) itacheza mechi mbili za mchujo za Kombe la Dunia, na baada ya Ngao ya Jamii, klabu za Tanzania zitacheza mechi za raundi ya awali ya mashindano ya ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.