Filamu ya ‘Last Stand’kufungua pazia la ZIFF 2025

DAR ES SALAAM: FILAMU kutoka nchini Uganda, ‘The Last Stand’ iliyoongozwa na Matt Bish ndiyo itakayofungua pazia la maonesho ya filamu Juni 25 mwaka huu wa 2025 wakati Tamasha la 28 la Kimataifa la Filamu Zanzibar (ZIFF) litakapozinduliwa kwa msimu mpya kuanzia Juni 25 hadi 29, 2025.
Filamu hiyo itakayooneshwa Ngome Kongwe huko Mji Mkongwe viziwani Zanzibar inayoelezea mambo yaliyomtokea kiongozi mmoja wa dini nchini Uganda wakati wa utawala wa Iddi Amin Dada ambapo kiongozi huyo alipambana na bila kuogopa vitisho vya kiongozi wa zamani wa Uganda Idd Amini.
Filamu hiyo imeeleza mambo mengi ambayo hayajulikani lakini yalitokea kwa Kiongozi huyo wa dini na Nduli Iddi Amini licha ya familia ya kiongozi huyo wa dini kumtaka kutompinga rais wa Uganda kwa kipindi hicho lakini yeye alibaki na msimamo wake wa kukemea mabaya yote aliyotenda Idd Amini.
Mtendaji Mkuu wa ZIFF, Joseph Mwale amesema tamasha hilo litaanza kwa maandamano ya ufunguzi kutoka kisonge hadi viwanja vya Ngome Kongwe kisha shindano la Mbio za Ngalawa litafanyika. Uoneshwaji wa filamu katika kumbi mbalimbali pia utafanyika na mwisho kutakuwa na usiku wa tuzo ambao utafanyika siku Juni 29 kisha itatangazwa tarehe mpya ya tamasha hilo kwa mwakani.
Naye Mkurugenzi wa Tamasha la ZIFF, Hatibu Madudu amesema wamepokea jumla ya filamu 430 ambapo filamu 174 zinatoka nchi za Afrika Mshariki na nyingine zimetoka nchi nyingine nje ya Afrika Mashariki.
Amezitaja baadhi ya nchi zilizowasilisha filamu zao kwa ajili ya kushindanisha katika tamasha hilo ni pamoja na filamu 49 kutoka Tanzania, filamu 54 kutoka Kenya, filamu 52 kutoka Uganda, filamu 6 kutoka Rwanda, filamu moja kutoka Burundi, filamu 4 kutoka Congo DRC na filamu 8 kutoka Somalia.
Filamu nyingine ni kutoka Irani ambapo wamewasilisha filamu 79, wakati Afrika Kusini wamewasilisha filamu 20 na filamu 36 zinatoka Misri. Filamu nyingine zimepokelewa kutoka nchi mbalimbali ikiwemo India, Brazil, Marekani, China, Italy, Uturuki, Nigeria, Argentina, Canada, Spain, Ureno, Zimbambwe, Arabuni, Ethiopia, mOROCCO, bURKINAFASO, gHANA, sENEGAR NA Ethiopia.
Maduhu amesema katika filamu walizopokea zipo ambazo hazitashindanishwa na nyingine katika tuzo licha ya kuoneshwa katika kumbi za tamasha hilo lakini vigezo vyake havijakidhi kwa ajili ya kushindanishwa hivyo wamezipa heshima ya kuoneshwa ili waweze kujifunza zaidia kwa lengo la kuboresha filamu zao zijazo.
Nao watengenezaji wa filamu Cecilia Lubango na filamu yake ya ‘Tears in the Rain’ na Sama Jahanpoor na filamu yake ya ‘My Dream’ ambao wote ni kutoka Tanzania wameeleza furaha yao na namna walivyopokea taarifa kuhusu filamu zao kuwa miongoni mwa filamu zitakazooneshwa katika tamasha la ZIFF 2025.
Naye mmoja wa waigizaji bora wa kike anayeshikilia tuzo za ZIFF mwaka 2022/2023 Tunu Mbegu ambaye kwa mwaka huu ataonekana kupitia filamu ya ‘Niko Sawa’ iliyoongozwa na Neema Ndepanya amesema filamu hii itaoneshwa kwa mara ya kwanza katika tamasha la ziff na filamu hiyo inagusa moja kwa moja jamii ambayo inachangamoto ya afya ya akili.




