‘Tshabalala’ aitaka nusu fainali Afrika
NAHODHA msaidizi wa timu ya soka ya Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ametamba kwamba kipaumbele cha kwanza cha timu yake msimu huu ni kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza na Spotileo ‘Tshabalala’amesema maandalizi na mbinu wanazopewa na kocha Juma Mgunda vinawapa jeuri ya kuamini watafika hatua hiyo ambayo imekuwa kikwazo kwao kwa misimu kadhaa iliyopita.
“Wachezaji wote tumekubaliana kuhakikisha tunaweka nguvu kubwa kwenye michuano ya CAF, ili kufika hatua ya nusu fainali msimu huu, ndio kiu yetu kubwa,” amesema ‘Tshabalala’.
Amesema dhamira kubwa ni kutaka kuboresha rekodi ya Simba katika michuano hiyo.
Kwa misimu mitatu mfululizo, mara mbili ligi ya mabingwa na moja Kombe la Shirikisho Simba imekua ikiishia hatua ya robo fainali ya michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika(CAF).




