Saka aibua mjadala kuhusu mpinzani wa Fainali ya Ulaya

LONDON: NYOTA wa Arsenal, Bukayo Saka, amewaacha mashabiki wa soka kwenye sintofahamu baada ya kutoa kauli ya fumbo akidai kuwa timu hiyo ina mpinzani inayomtaka kwa ajili ya fainali ya UEFA Champions League msimu huu.
Saka mwenye umri wa miaka 24 aliihakikishia Arsenal tiketi ya kufika fainali hiyo itakayofanyika Budapest baada ya kufunga bao katika ushindi wa jumla wa mabao 2-1 dhidi ya Atletico Madrid katika nusu fainali.

Hii ni mara ya kwanza kwa Arsenal kufika hatua hiyo ndani ya miaka 20 tangu walipopoteza dhidi ya Barcelona mwaka 2006 chini ya kocha Arsene Wenger.
Katika fainali hiyo, Arsenal itakutana na mshindi kati ya Paris Saint-Germain au Bayern Munich, huku PSG ikiwa na faida ya mabao 5-4 kufuatia mchezo wa kwanza.
Alipoulizwa ni timu ipi angependa kukutana nayo fainali, Saka alijibu kwa njia ya mafumbo akisema:
” Kuniuliza hilo, najua nitalazimika kutoa jibu la kawaida la vyombo vya habari… lakini ndani kabisa unajua ni nani tungependa kukutana naye, hicho tu ndicho nasema.”
Kauli hiyo imezua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki, baadhi wakiamini Arsenal inaweza kutaka kulipiza kisasi dhidi ya PSG waliowaondoa msimu uliopita, huku wengine wakihisi Bayern Munich inaweza kuwa chaguo kutokana na historia yao, licha ya uwepo wa mshambuliaji Harry Kane ambaye aliwahi kung’ara kwa watani wao Tottenham Hotspur.
Kwa upande wake, nguli wa Arsenal Ian Wright aliwataka mashabiki kufurahia mafanikio hayo, akisisitiza kuwa ni hatua kubwa kwa klabu hiyo.
Naye kocha wa zamani wa Arsenal, Wenger, alieleza kuwa furaha hiyo ni halali lakini akasisitiza umuhimu wa kuelekeza nguvu katika fainali ijayo.
Sasa macho yote yanaelekezwa Mei 30, ambapo Arsenal itashuka dimbani kusaka historia mpya barani Ulaya.




