Simba Queens yachimbwa mkwara
DODOMA: UONGOZI wa Fountain Gate Princess umeweka wazi kuwa msimu ujao wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania, hawatakuwa wanyonge na kufuta ufalme wa timu mbili, Simba Queens na JKT Queens, zimekuwa zikitawala katika ligi hiyo.
Afisa Habari wa Fountain Gate Princess, Issa Mbuzi amesema hivi karibuni baada ya kukamilika kwa msimu wa 2023\24, wamevunja benchi la ufundi, wakati wowote kuanzia sasa wanatarajia kutangaza benchi jipya.
Kuhusu aliyekuwa Kocha wa Yanga Princess na Biashara United, Edma Lema kuhusishwa kwenda kukinoa kikosi cha timu hiyo, amesema hakuna ukweli juu ya mwalimu huyo licha ya kudai kuwa kocha wao atakuwa mtanzania.
“Hakuna ukweli juu ya Edna, tupo kwenye mazungumzo na mmoja ya kocha mzawa na tutamtambulisha muda wowote kuanzia sasa, baada ya kukamilisha tunaendelea na usajili kwa kufuata mapendekezo ya timu yetu kwa msimu ujao,” amesema Mbuzi.
Amesema wanaangalia nafasi tatu katika usajili huo, kiungo mkabaji, beki na mshambuliaji ambao wanaimani watasajili watu wa maana na kuongeza nguvu kwenye timu hiyo na kufanya mageuzi msimu ujao.
Mbuzi amesema wanahitaji kuwa bora na kufuta ufalme wa klabu mbili kubwa Simba Queens na JKT Queens wakionyesha ubabe wa kila msimu kupokezana kutwaa taji la ubingwa wa Ligi hiyo, kwa msimu ujao kuongeza ushindani mkubwa katika mbio za ubingwa.