Nonini alipwa fidia ya milioni 4 za Kenya, Mutinda apinga
NAIROBI: MTAYARISHAJI wa maudhui Brian Mutinda amewasilisha rufaa katika Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa Mahakama ya Milimani uliompa mwanamuziki Hubert Nakitare maarufu ‘Nonini’ milioni 4 za Kenya katika kesi ya kukiuka hakimiliki.
Uamuzi huo uliotolewa mwezi uliopita na Hakimu Mkuu, Hosea Ng’ang’a, ulimpata Mutinda na Syinix Electronics Ltd na hatia ya kutumia wimbo wa Nonini ‘Wee Kamu’ kwenye tangazo la mtandaoni bila idhini yake.
Rufaa ya Mutinda, iliyowasilishwa kwa Mahakama Kuu mnamo Oktoba 3, 2024, inaeleza sababu 12 za malalamiko, ikiwa ni pamoja na fidia ya Shilingi milioni 4 za Kenya alizopata.
Katika nyaraka zake mahakamani, Mutinda anahoji, “Hakimu alikosea kisheria kumpa mlalamikiwa fidia ya jumla ya Ksh 4,000,000 bila mshitaki ambaye ni Nonini kutoa ushahidi wowote wa fidia iliyotokana na ukiukaji huo.
Awali, Nonini alipewa fidia ya Shilingi milioni 1 mnamo Machi 23, lakini uamuzi huo ulibatilishwa baada ya Mutinda kukata rufaa, akidai hakupewa fursa ya kujitetea.
Mahakama ilimruhusu Mutinda kuwasilisha tena utetezi wake, ambao ulizingatiwa katika kesi iliyofuata, na kusababisha kuongezwa kwa tuzo ya Sh milioni 4.
Mutinda anapinga ongezeko hilo, akisema, “Hakimu msomi alikosea kisheria na ukweli kwa kuongeza fidia ya awali kutoka fedha za Kenya 1,000,000 hadi 4,000,000 baada ya kusikilizwa kwa kesi baina ya pande zote, bila mlalamikaji kuwasilisha ushahidi wowote wa ziada.
Katika uamuzi wake, Hakimu Mkuu Ng’ang’a alishughulikia masuala muhimu, ikiwa ni pamoja na kubaini umiliki wa Nonini wa hakimiliki ya wimbo husika na kubainisha ni nani aliyehusika kuchapisha video inayokiuka. Aligundua kuwa Nonini ndiye anamiliki hakimiliki hiyo na kwamba kampuni ya Syinix Electronics Ltd ilichapisha video hiyo, huku Mutinda akishindwa kutoa ushahidi unaoonesha kuwa ushiriki wake ulikuwa wa kutoa video mbichi bila muziki huo. Kwa hivyo mahakama iliwawajibisha Mutinda na Syinix kwa ukiukaji huo.