Ligi Kuu

Barker: Tunajua ugumu wa Pamba, tutapambana

MWANZA: KOCHA Mkuu wa Simba, Steven Barker, amesema mchezo wa kesho dhidi ya Pamba Jiji utakuwa miongoni mwa mechi ngumu kwa timu yake, akieleza kuwa uzoefu walioupata msimu uliopita umewasaidia kujua namna ya kukabiliana na changamoto watakazokutana nazo.

Simba itashuka dimbani kesho, Jumatano, Agosti 19, 2026, dhidi ya Pamba Jiji katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, ikiwa ni mchezo wake wa pili wa Ligi Kuu msimu huu. Simba ilianza kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Barker amesema kumbukumbu ya mchezo wa msimu uliopita ugenini dhidi ya Pamba Jiji, uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, umewapa somo muhimu kabla ya kurejea Mwanza.

“Uzoefu wa kucheza ugenini dhidi ya Pamba msimu uliopita ulikuwa miongoni mwa mechi ngumu zaidi kwetu. Tumejifunza mengi na sasa tunajua vizuri zaidi kile tunachotarajia,” amesema Barker.

Kocha huyo amesema licha ya changamoto hiyo, Simba haina budi kutafuta suluhisho ikiwa inataka kuendelea kushinda na kujiweka katika nafasi nzuri juu ya msimamo wa ligi.

Barker pia amedokeza kuwa usajili wa Kevin Nashon, aliyewahi kuichezea Pamba Jiji, unaweza kuwa na manufaa kwa Simba kutokana na taarifa alizonazo kuhusu wapinzani hao.

Kocha Msaidizi wa Pamba Jiji John Wawu amesema amewaandaa wachezaji wake vizuri kwa ajili ya mchezo wa kesho, anaamini matokeo yatakuwa upande wao.

Pamba Jiji imetoka kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Dodoma Jiji katika mchezo uliopita.

Related Articles

Back to top button