Mwamnyeto: Yanga hatukukata tamaa

DAR ES SALAAM: NAHODHA wa Yanga, Bakari Mwamnyeto, amesema nidhamu na kutokata tamaa kuliwasaidia kusawazisha na kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya watani wao Simba katika dabi ya Kariakoo.
Mwamnyeto, ambaye ndiye aliyefunga bao la kusawazisha katika mchezo huo, amesema walikutana na upinzani mkali huku wapinzani wao wakitangulia kuongoza kabla ya wao kurejea mchezoni.
“Mchezo ulikuwa mgumu, watani zetu walitangulia kupata matokeo na kuongoza mabao 2-1, lakini baada ya mapumziko mwalimu alituambia tusikate tamaa,” amesema.
Amesema kuwa maelekezo ya benchi la ufundi pamoja na utayari wa wachezaji vilichangia kubadili matokeo na kufanikisha kusawazisha.
“Baada ya kurudi kipindi cha pili tulijipanga vizuri na kufanikiwa kusawazisha. Sisi kama wachezaji tulikuwa tayari tangu tukiwa Zanzibar, hivyo tulijua nini cha kufanya ndani ya uwanja,” alieleza.
Nahodha huyo alibainisha kuwa matokeo hayo yanaendelea kuwaweka Yanga katika nafasi nzuri ya ushindani, akisisitiza kuwa wana tofauti ya pointi tano dhidi ya wapinzani wao na wataendelea kujipanga kwa michezo ijayo.




