Mkude atambulishwa Mashujaa

KIGOMA: KIUNGO mkongwe Jonas Mkude amejiunga na Mashujaa FC kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akirejea kwenye ushindani wa ligi baada ya kupitia klabu kubwa mbili nchini, Simba na Yanga.
Mkude, ambaye ni miongoni mwa viungo wenye uzoefu mkubwa katika soka la Tanzania, amekuwa na safari ndefu kwenye soka la ushindani, akijenga jina kubwa zaidi wakati akiitumikia Simba, kabla ya baadaye kujiunga na Yanga.
Uzoefu wake wa kucheza katika mechi kubwa na mashindano ya ndani na kimataifa unatarajiwa kuwa nyongeza muhimu kwa Mashujaa, ambao wameendelea kujenga kikosi chenye mchanganyiko wa wachezaji vijana na wenye uzoefu.
Akiwa Simba, Mkude alifanikiwa kubeba mataji kadhaa ya Ligi Kuu pamoja na kushiriki katika mashindano ya CAF, huku akiwa miongoni mwa viungo waliodumu kwa muda mrefu kwenye kikosi hicho.
Baada ya kuondoka Simba, kiungo huyo alijiunga na Yanga, hivyo kuwa miongoni mwa wachezaji wachache waliowahi kuvaa jezi za vigogo hao wawili wa soka la Tanzania.
Ujio wake Mashujaa unatarajiwa kuongeza ushindani katika eneo la kiungo, huku uzoefu wake ukitarajiwa kusaidia timu hiyo katika harakati zake za kufanya vizuri kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu.
Kwa Mashujaa, usajili wa Mkude pia unaweza kuwa fursa ya kupata kiongozi ndani ya uwanja kutokana na uzoefu wake wa kucheza katika mazingira yenye presha na mechi kubwa.




