Yanga yatangaza tenda ya ujenzi wa jengo la ghorofa 12

DAR ES SALAAM: UONGOZI wa Yanga umetangaza tenda kwa makampuni yenye sifa, uzoefu na uwezo katika sekta ya ujenzi kwa ajili ya kushirikiana na klabu hiyo katika ujenzi wa jengo la ghorofa 12 linalomilikiwa na klabu hiyo.
Jengo hilo lipo katika eneo la Mtaa wa Mafia na Nyamwezi, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa tangazo la klabu hiyo lililotolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu Andre Mtine, kampuni zenye nia ya kushiriki katika tenda hiyo zinatakiwa kufika Makao Makuu ya Yanga kwa ajili ya kununua na kuchukua Kitabu cha Tenda (Tender Document), kitakachokuwa na maelekezo, vigezo na masharti ya kushiriki katika mchakato huo.
Yanga imeeleza kuwa maombi pamoja na nyaraka zote zinazohitajika, kwa mujibu wa Kitabu cha Tenda, zinapaswa kuwasilishwa kupitia njia iliyoainishwa katika kitabu hicho.
Mwisho wa kuchukua na kuwasilisha Kitabu cha Tenda ni Jumanne, Septemba 1, 2026, huku maombi yatakayowasilishwa baada ya muda huo yakielezwa kutopokelewa.




