Ligi Kuu

Yanga yaipiga chenga Simba

MWANZA: OFISA Habari wa Yanga, Ali Kamwe, ameweka wazi kuwa timu yake haitaki kujiwekea presha kwa kufikiria zaidi mchezo wa Kariakoo Derby, badala yake wanajikita kikamilifu katika mechi yao ya kesho ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Pamba Jiji FC.

Yanga watakuwa ugenini katika mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Kamwe amesema licha ya mashabiki na wadau wa soka kuzungumzia Kariakoo Derby, wao wanazingatia zaidi mchezo wao wa ligi dhidi ya Pamba.

“Hatutaki kujitia presha kwa kuwaza Kariakoo Derby. Hatutachukua ubingwa kwa kushinda mechi moja pekee, tunapaswa kushinda kila mchezo kabla ya kumkabili mpinzani wetu, Simba, Machi 8.

“Tumejifunza kutokana na makosa ya nyuma. Tukumbuke kuwa Simba walitoka sare dhidi ya Fountain Gate FC kule Manyara, na baadaye sisi tukatoka sare na JKT Tanzania.

Hili linapaswa kuwa funzo kwetu. Simba wametoka sare na Azam FC, lakini hatupaswi kuwachukulia kwamba wametoka kwenye mbio za ubingwa. Bado tuna mechi ngumu mbele yetu,” alisema Kamwe.

Pia alisisitiza kuwa wanapaswa kuzingatia mchezo wao wa Ijumaa, Februari 28, dhidi ya Pamba Jiji FC  timu nzuri wanajikita kwa mchezo huo, badala ya kufuatilia sare ya Simba na Azam FC.

“Tunahitaji kushinda huu mchezo na kupata alama tatu. Sio lazima tucheze soka la kuvutia au tufunge mabao mengi huku tukiruhusu mabao mengi pia. Mwisho wa siku kinachoangaliwa ni alama tatu, siyo urembo wa mpira,” aliongeza Kamwe.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button