Ligi Kuu

Yanga ni mwendo wa damu changa

DAR ES SALAAM: YANGA imeanza kuonesha mwelekeo mpya katika dirisha hili la usajili kwa kuhamishia nguvu zake kwa nyota vijana wanaong’ara Ligi Kuu Bara, hatua inayoonekana kulenga kujenga kikosi imara cha sasa na baadaye.

Mabingwa hao watetezi tayari wamemtangaza kiungo Abdulnasr Muhamed aliyekuwa Mashujaa FC, ambaye kabla ya hapo aliichezea Mlandege na kuvutia kutokana na kiwango chake.

Mbali na Abdulnasr, Yanga pia imemtambulisha Hussein Mihambo akitokea timu ya vijana ya Mashujaa FC. Msimu uliopita Mihambo alikuwa miongoni mwa wachezaji waliovutia zaidi baada ya kuibuka mchezaji bora katika mechi kadhaa kutokana na kiwango chake.

Usajili huo unamfanya Mihambo kuwa kijana wa tatu kutua Jangwani katika dirisha hili, baada ya Yanga hivi karibuni kumsajili Juma Issa maarufu ‘Chuga Boy’ kutoka Fountain Gate.

Chuga Boy alikuwa miongoni mwa wachezaji waliotikisa Ligi Kuu msimu uliopita kwa kiwango chake bora, hali iliyomfanya ahusishwe na klabu mbalimbali za Ulaya kabla ya Yanga kufanikisha usajili wake.

Mwelekeo huo wa Yanga unaonesha klabu hiyo imeamua kuwekeza zaidi kwenye vipaji vya ndani vinavyotarajiwa kuwa mhimili wa kikosi chake katika misimu ijayo, huku ikichanganya uzoefu wa nyota wakubwa na nguvu ya damu changa kuelekea msimu mpya wa mashindano.

Bado mashabiki wa klabu hiyo wanatamani kusikia majina makubwa kutoka mataifa mengine kuboresha kikosi chake kwa ajili ya Ligi Kuu sambamba na mashindano ya kimataifa.

Related Articles

Back to top button