Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema klabu hiyo ni kubwa hivyo inapaswa kushinda michezo yake ukiwemo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC Agosti 23.
Amesema hayo leo wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo wa kwanza kwa Yanga kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
“Ratiba ni kweli ni ngumu kutokana na ratiba ya michezo kuwa mingi lakini hiyo ndio kazi yetu. Tunapaswa kujiandaa kama timu kubwa ili kupata matokeo chanya katika kila mechi,”amesema Gamondi.
Amewaahidi mashabiki wa Yanga kwamba timu hiyo itacheza kandanda safi na la kuvutia ili kupata matokeo na kwamba imejipanga na imejiandaa kuwapa burudani.
Kocha huyo amesema kulikuwa na shida kwa wachezaji kadhaa, watawaangaliwa kwenye mazoezi ya leo kuona kama wanaweza kutumika kesho lakini kiujumla afya za wachezaji zipo imara na wana utayari wa kucheza mchezo huo.