Khaligraph Jones, Femi One waibuka kwenye mashindano ya Rugby Sevens

NAIROBI: WASANII maarufu wa Kenya, Khaligraph Jones, Femi One na Dyana Cods, wametoa burudani kwa mashabiki wao wakati wa mashindano ya Rugby Sevens, yaani mchezo wa raga unaochezwa na wachezaji saba kwa kila timu, badala ya wachezaji 15 wa kawaida.
Mashindano hayo ya rugby yalifikia tamati katika viwanja vya RFUEA Grounds, huku muziki na burudani vikiwa vimeongoza hamasa kwa mashabiki waliojitokeza kushuhudia hatua ya mwisho ya mchezo huo wa taifa kwa mwaka 2026.
Khaligraph Jones ndiye aliyekuwa kivutio kikuu cha burudani. Msanii huyo alitumbuiza baadhi ya nyimbo zake maarufu, akisaidiwa na DJ Schwaz, DJ Ruffi na DJ Sanif.
Wasanii wengine waliotumbuiza katika mashindano hayo ni MC BV Accurate, Dyana Cods na Femi One, ambao walipanda jukwaani na kutoa burudani ya nguvu huku DJs Nickdee, Pinto na Verah wakisaidia kusherehesha kwa midundo moto moto na MC BV Accurate ndiye alikuwa muongoza sherehe hizo.
Burudani hiyo ilikuwa sehemu ya Tusker na Rugby, mpango uliounganisha muziki na burudani katika hatua zote sita za ‘National Sevens Circuit’ zilizofanyika Nakuru, Kisumu, Nairobi, Mombasa na Embu.
Kwa upande wa washindi wa rugby, KCB Rugby ilitetea ubingwa wa ‘National Sevens Circuit’ kwa msimu wa tatu mfululizo.




