Afrika Mashariki

Mahakama yakataa ombi la muigizaji kujiondoa kwenye kesi ya haki miliki

Nairobi: Mahakama nchini Kenya imekataa ombi la mwigizaji na mtayarishaji wa maudhui Foi Wambui la kutaka kuondolewa katika kesi ya ukiukaji wa hakimiliki inayohusisha matumizi ya wimbo wa mwanamuziki Joseph Mwaura Mutoriah, maarufu kama Mutoriah.

Kesi hiyo inatokana na matumizi ya wimbo ‘Beta’ katika video ya matangazo iliyohusishwa na kampeni ya simu ya OPPO Reno 12 5G. Mutoriah alidai kuwa wimbo huo ulitumika katika video bila kupata leseni ya ‘synchronisation’, ambayo huhitajika wakati muziki unapounganishwa na picha au video kwa matumizi ya kibiashara.

Kwa mujibu wa taarifa za awali za kesi hiyo, video hiyo iliwekwa kwenye ukurasa wa Wambui kwenye Instagram na baadaye OPPO Kenya ikaikuza kama maudhui ya kulipiwa (sponsored content) kwa kipindi cha siku sita. Mutoriah alidai kuwa matumizi hayo yalifanyika bila idhini yake kama mwenye haki za kazi hiyo.

Mutoriah aliwasilisha madai dhidi ya Wambui, OPPO Kenya pamoja na kampuni ya masoko ya Aifluence Ltd, akitaka kulindwa kwa haki zake za ubunifu na kulipwa fidia kwa matumizi ya kazi yake bila ruhusa.

Taarifa nyingine ziliripoti kuwa Wambui alikuwa amelipwa takribani Sh600,000 kwa sehemu yake katika dili hilo la kibiashara.

Kabla ya shauri kufikishwa mahakamani, pande hizo zilijaribu kufikia suluhu nje ya mahakama. Menejimenti ya Wambui iliripotiwa kutoa ofa ya Sh50,000 kama sehemu ya makubaliano, lakini Mutoriah aliikataa akisema kiasi hicho hakikulingana na thamani ya haki miliki yake.

Kwa kukataa ombi la Wambui la kujiondoa kwenye kesi, mahakama imeacha shauri hilo liendelee huku pande zinazohusika zikiendelea kuwasilisha hoja zao kuhusu matumizi ya wimbo huo na uwajibikaji wa wahusika katika kampeni hiyo ya kibiashara.

Kesi hiyo imeibua mjadala mpana kuhusu umuhimu wa wasanii, waandaaji wa maudhui na makampuni kuhakikisha wanapata vibali sahihi kabla ya kutumia muziki wenye hakimiliki katika matangazo na maudhui ya kibiashara.

Related Articles

Back to top button