Yanga kuwavaa Stand United, Simba kukutana na Mbeya City robo fainali CRDB

DAR ES SALAAM: DROO ya robo fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB BANK imekamilika, ambapo mabingwa watetezi Yanga SC watamenyana na Stand United, huku Simba SC wakipangwa dhidi ya Mbeya City, timu iliyowatoa Azam FC katika hatua ya 16 bora.
Mbeya City, inayoshiriki Ligi ya Championship, imekuwa moja ya timu zinazoshangaza msimu huu baada ya kuwaondoa Azam FC, na sasa wanakutana na Simba katika pambano linalotarajiwa kuwa na ushindani mkali.
Katika mechi nyingine, JKT Tanzania watapambana na Pamba Jiji FC, huku Singida Black Stars wakikabiliana na Kagera Sugar.
Kwa mujibu wa ratiba, mshindi kati ya Yanga na Stand United atakutana na mshindi wa mchezo kati ya JKT Tanzania na Pamba Jiji FC katika hatua ya nusu fainali.
Vilevile, mshindi wa pambano la Simba na Mbeya City atamenyana na mshindi wa mchezo wa Singida Black Stars dhidi ya Kagera Sugar.
Mechi za robo fainali zinatarajiwa kuchezwa kati ya Aprili 11 – 13, huku nusu fainali ikipangwa kupigwa kati ya Aprili 25 – 27.
Michuano hii inaendelea kuwa na ushindani mkubwa, huku timu zote zikilenga kutwaa taji la CRDB BANK msimu huu.