Wolper awaza kesho ya wanae

DAR ES SALAAM: MSANII wa filamu za nchini, Jackline Wolper amesema hana haraka ya kutafuta maisha ya kifahari, kwani anachokipa kipaumbele ni watoto wake kupata malezi na msingi imara wa maisha yao ya baadaye.
“Sijawahi kufikiri kuwa nikifikisha umri fulani niwe na maisha ya namna fulani au ya kifahari. Kwa sasa nina watoto wananiangalia mimi,” amesema Wolper.

“Mimi najali zaidi watoto wangu. Haya mambo ya watu kusema mtoto atajipambania mwenyewe si sawa kabisa. Kama mzazi, unapaswa kupambania kesho ya mtoto wako iwe bora,” amesisitiza.
Aidha, Wolper amesema nyumba yake haijakamilika kama ambavyo watu wanadhani.
“Ukweli ni kwamba ndani bado haijakamilika. Hata makochi sina, wala kitanda sina. Watoto wanalala chini kwenye godoro, na mimi pamoja na mume wangu tunalala chini kwenye godoro. Hatuna haraka ya maisha, mambo yetu tunayafanya polepole lakini kwa uhakika,” amefafanua.
Kauli hiyo imeonyesha upande mwingine wa maisha ya msanii huyo, akisisitiza kuwa mafanikio ya kweli kwake ni kuona watoto wake wanakuwa katika mazingira bora, hata kama ni kwa hatua ndogo ndogo.




