Wasanii wanaotaka kutumbuiza Sauti za Busara 2027 dirisha limefunguliwa

ZANZIBAR : WAANDAAJI WA Tamasha la Kimataifa la Muziki la Sauti za Busara linalofanyika kila mwaka visiwani Zanzibar wamesema zimebaki wiki mbili pekee kabla ya kufungwa kwa dirisha la maombi ya wasanii wanaotaka kushiriki katika Tamasha hilo kwa mwaka 2027.
Pia waandaaji hao wamewataka wasanii wa ndani ya Afrika na na wale wa kutoka nje diaspora kuwasilisha maombi yao mapema.
Mwisho wa kupokea maombi ni Juni 30, 2026. Wasanii na wadau wa sanaa wamehimizwa kuomba mapema ili wapate mud awa kujiandaa wa kutosha kushiriki tamasha hilo.
Tamasha hilo, ambalo ni miongoni mwa matukio makubwa na yanayoheshimika zaidi ya muziki barani Afrika, linatarajiwa kufanyika visiwani Zanzibar kuanzia Machi 19 hadi 21, 2027.
Kwa mujibu wa waandaaji, jukwaa la toleo la 24 la tamasha hilo linakaribisha wabunifu wa utamaduni, vinara wa mabadiliko na wasimuliaji wa hadithi kupitia muziki ili kuonesha vipaji vyao mbele ya hadhira ya kimataifa.
Waandaaji wameeleza kuwa kipaumbele kitatolewa kwa muziki wa Afrika na diaspora ni msanii anayeweza kuimba live kwa asilimia 100, pamoja na vikundi vya wanawake au vinavyoongozwa na wanawake, sambamba na vipaji vipya vinavyochipukia.




