Riadha

Wanariadha wa Tanzania wang’ara Kili Half Marathon 2026

KILIMANJARO: Wanariadha wa Tanzania wameendelea kuonesha kiwango cha juu cha ushindani katika mashindano ya Kili International Half Marathon 2026.

Mashindano hayo ya kilomita 21, ambayo ni sehemu ya tamasha kubwa la kila mwaka la Kili International Marathon, yameendelea kuwa jukwaa la kuhamasisha afya kupitia mazoezi pamoja na kukuza vipaji vya wanariadha wa ndani na nje ya nchi.

Katika matokeo ya mwaka huu, upande wa wanaume ulitawaliwa na Michael Geay aliyenyakua medali ya dhahabu baada ya kumaliza mbio kwa muda wa saa 1:04:10.

Alifuatiwa kwa karibu na Josephat Joshua Gisumo aliyetumia saa 1:04:14, huku James Kairuki raia wa Kenya akishika nafasi ya tatu kwa muda wa saa 1:04:30.

Kwa upande wa wanawake, Hamida Musa aliibuka kinara akifuatiwa na Failuna Matanga wote kutoka Tanzania, huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Veronika Wanjiku raia Kenya.

Akizungumzia ushindi wake, Geay amesema kuwa ushindani ulikuwa mkali, lakini alijivunia kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.

“Nimefurahi sana kushinda. Haikuwa rahisi, kwani kila mmoja alikuwa analenga medali ya dhahabu,” amesema Geay.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, aliwapongeza wanariadha hao kwa nidhamu, uzalendo na jitihada zao. Aidha, alisoma salamu za pongezi kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameahidi kuwa mgeni rasmi katika mashindano ya mwakani pamoja na kuongeza zawadi kwa washindi hadi kufikia shilingi milioni 100.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Yas, Pierre Canton Bacara alisema ushindani wa mashindano hayo unaendelea kuongezeka kila mwaka, huku akisisitiza dhamira ya kampuni hiyo katika kuendeleza michezo, kuimarisha uhusiano na jamii pamoja na kulinda mazingira kupitia miradi ya upandaji miti zaidi ya 50,000 katika maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro.

Ameongeza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu ya “Kila Kona, Kila Hatua Kasi zaidi” inalenga kuonesha jitihada za kusambaza huduma za mawasiliano ya 4G na 5G nchini kote. Pia alibainisha kuwa kampuni hiyo imeendelea kutambuliwa kimataifa kwa ubora wa mtandao wake.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, aliipongeza Yas kwa mchango wake katika maendeleo ya jamii, akieleza kuwa mashindano hayo yamekuwa chachu ya kukuza utalii, biashara na uchumi wa mkoa huo.

Maelfu ya washiriki na mashabiki walijitokeza kushiriki na kushuhudia mashindano hayo, huku wanariadha wa Tanzania wakionekana kutawala ushindi katika makundi mbalimbali jambo lililozua hamasa kwa wananchi.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button