Muziki

Serikali kugharamia matibabu ya Mkubwa Fella

DAR ES SAALAAM: WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema Serikali itaanza kugharamia matibabu ya mdau wa muziki, Saidi Fella maarufu kama Mkubwa Fella, ambaye ana changamoto ya kiafya kwa muda mrefu.

Makonda alitoa tamko hilo alipokutana na wasanii wa Bongo Fleva wanaojiandaa na tamasha la maadhimisho ya miaka 30 ya muziki huo, baada ya kupongeza hatua yao ya kumtembelea na kumjulia hali Mkubwa Fella.

Kauli ya Makonda inakuja baada ya wasanii hao kuwasilisha maombi ya Babu Fella aliyeomba kusaidiwa vifaa vya mazoezi pamoja na usafiri kwa ajili ya kumpeleka hospitali kila siku.

Amesema kitendo cha wasanii hao kimeonesha mshikamano na kuthamini mchango wa watu walioweka msingi wa maendeleo ya tasnia ya muziki nchini.

Baada ya kufahamishwa kuhusu hali ya afya ya Mkubwa Fella na changamoto zinazomkabili, Makonda amesema Serikali haitamuacha peke yake.

“Kuanzia sasa Serikali itagharamia matibabu ya Mkubwa Fella. Tutafanya utaratibu kupitia wizara kuhakikisha anapata matibabu na uangalizi unaostahili,” amesema Makonda.

Amesema Babu Fella ni mmoja wa wadau waliotoa mchango mkubwa katika kukuza muziki wa kizazi kipya kwa kuwaibua na kuwalea wasanii wengi waliokuja kuwa nyota wa Bongo Fleva.

Makonda amesema ni wajibu wa serikali kuthamini na kuwatunza watu waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sanaa nchini, hasa wanapokumbwa na changamoto za kiafya.

Related Articles

Back to top button