Waitara NBC Trophy yavuta wachezaji 147

DAR ES SALAAM: Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu Lugalo, Brigedia Jenerali mstaafu Michael Luwongo, amesema shindano la Waitara NBC Trophy limefanikiwa baada ya kuvutia wachezaji 147 waliokuwepo kushiriki katika vipengele tofauti.
Kivutio kikubwa zaidi katika shindano hilo ni mshindi wa jumla, ambaye ni mtu mzima ukilinganisha na idadi kubwa ya washiriki waliokuwa vijana.
Mshindi huyo wa jumla alikuwa Dk. Edmund Mndolwa, aliyepata pointi za juu kwa kushinda Gross 78, HCP 12 na Net 66. Hata yeye mwenyewe hakuamini ushindi huo na alisema ataonesha wajukuu zake kombe alilopata.
Luwongo alisema shindano hilo, lililoandaliwa kwa heshima ya Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali George Waitara, lilipaswa kufanyika mwaka jana, lakini kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao, hawakufanikiwa kulifanya. Hivyo, lilifanyika mwishoni mwa wiki na tayari amethibitisha kuwa lingine litafanyika tena baadaye.
“Tumepata mafanikio kwa sababu washiriki wamekuwa wengi katika vipengele tofauti, lakini mwisho wa siku washindi ni wachache. Tunawapongeza wote walioshiriki, wakiwemo watoto, vijana, wanawake na wazee,” amesema.
Jenerali Waitara ni muasisi wa Klabu ya Gofu ya Lugalo na ndiye aliyeanzisha viwanja vya kuchezea gofu vya Lugalo. Hivyo, wamekuwa wakimuenzi kwa kuandaa shindano hilo kila mwaka ili kuthamini mchango wake katika michezo nchini.