Africa

Wafcon 2026 yasogezwa mbele

CAIRO: SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limesogeza mbele mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON 2026) ikiwa zimesalia siku 12 kabla ya mashindano hayo kuanza nchini Morocco.

Awali mashindano hayo yalipangwa kufanyika kuanzia Machi 17 hadi Aprili 3 mwaka huu, sasa yatafanyika kuanzia Julai 25 hadi Agosti 16, mwaka huu.

CAF hawakuweka wazi sababu za kusogezwa mbele kwa mshindano hayo.

Michuano hiyo pia itatumika kutoa nafasi ya timu kufuzu michuano ya Kombe la Dunia kwa Wanawake 2027 itakayofanyika nchini Brazil.

Morocco ilipangwa kuwa mwenyeji wa fainali hizo kwa mara ya tatu mfululizo, lakini wiki za hivi karibuni kuliibuka tetesi kuhusu uwezekano wa kubadilishwa kwa mwenyeji, jambo lililozua minong’ono kwa wadau wa soka barani Afrika.

Tetesi hizo ziliongezeka baada ya matukio ya vurugu yaliyoripotiwa wakati wa fainali ya AFCON 2025 kwa upande wa wanaume, ambapo Morocco ilifungwa bao 1-0 na Senegal katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Stade Moulay Abdellah jijini Rabat.

CAF imesema maandalizi ya mashindano yanaendelea, ingawa bado haijaweka wazi kama Morocco itaendelea kuwa mwenyeji wa michuano hiyo.

 

 

Related Articles

Back to top button