Burudani

Wadau wajadili sanaa zenye staha

MOROGORO :WAKATI sekta ya sanaa na ubunifu ikiendelea kukua kwa kasi na kutoa ajira kwa maelfu ya vijana nchini, wadau wameonya kuwa bila kuwepo kwa kazi zenye staha, mchango wake katika kukuza uchumi wa Taifa unaweza kubaki kwenye takwimu zisizogusa maisha halisi ya wasanii.

Kauli hiyo imetolewa katika warsha ya siku tatu ya kusambaza matokeo ya utafiti kuhusu uendelezaji wa kazi zenye staha katika sekta ya utamaduni na uchumi wa ubunifu nchini Tanzania. Warsha hiyo imeandaliwa na Shirika la Kazi Duniani kwa ufadhili wa Norway.

Utafiti uliowasilishwa umebainisha kuwa licha ya sekta ya utamaduni na ubunifu kuongeza mchango wake katika pato la Taifa na ajira kwa vijana, ukuaji huo haujaambatana na ulinzi wa kijamii, mikataba rasmi wala mazingira salama ya kazi kwa wasanii wengi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Taasisi ya SEDEVA, Izack Abeneko, amesema pamoja na sekta hiyo kuwa chanzo kikubwa cha kipato na ajira hasa kwa vijana, bado kuna haja ya kuweka mifumo madhubuti ya kulinda haki za wasanii na kurasimisha shughuli zao.

“Mazingira ya kazi ya wasanii wengi bado si rasmi. Ni kazi za msimu au za hapa na pale; msanii hawezi kujua ni lini atapata kazi nyingine. Serikali inapaswa kuimarisha utekelezaji wa sheria zilizopo ili zilete matokeo chanya kwa wadau wa sanaa na kumpunguzia mzigo msanii huku akielewa thamani ya kulinda haki zake,” amesema Abeneko.

Related Articles

Back to top button