Wachezaji Gofu zaidi ya 120 kuchuana kesho

WACHEZAJI zaidi ya 120 wanatarajia kuchuana kesho katika shindano la siku moja litakalohusisha klabu tatu za Dar es Salaam Gymkhana, Morogoro na Lugalo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam Leo Katibu wa klabu ya Lugalo Luteni Kanali mstaafu Shabani Kitogo amesema shindano hilo linalodhaminiwa na CRDB litahusisha wachezaji wa ridhaa na wa kulipwa.
“Maandalizi yameshafanyika kinachosubiriwa ni wachezaji tu kuja kushiriki. Nawashukuru benki ya CRDB kwa kuwa mdhamini mara ya tatu mfululizo, naomba muendelee kuwa nasi katika kuinua mchezo huu,”amesema.
Mkuu wa kitengo cha huduma kwa wateja binafsi CRDB Stephen Adili amemshukuru uongozi wa Gofu wa Lugalo kwa kuendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha Watanzania wengi wanaingia katika mashindano hayo kwa kuwa ni ajira na huleta undugu.
“Pamoja na kutambua michezo ni lugha ya kimataifa ndio maana hata sisi tupo kimataifa ili wachezaji wanaoenda kimataifa tunakuwa pamoja nao. Nawakaribisha Watanzania wote katika mashindano yetu kesho na wengine waje wajifunze,”amesema.
Amesema mchezo huu ni kwa ajili ya rika zote, vipato vya aina zote hivyo, watu wajitokeze kushiriki mchezo huo na kuonesha vipaji vyao.
Nahodha Msaidizi wa Lugalo Gofu Klabu Samwel Mosha amesema shindano hilo litahusisha wachezaji mmoja mmoja ambapo wachezaji watajipambania wenyewe.
Amesema wachezaji wa kulipwa na ridhaa zaidi ya 120 tayari wamejiandikisha. Kutakuwa na Daraja la Kwanza, Daraja B, C, wanawake na wazee.
“Zawadi tayari tumeziandaa kwa ajili ya mashindano hayo ikiwemo fedha tasilim na vitu, niwashukuru CRDB kwa namna wanavyotushika mkono kusapoti mchezo huu,”amesema.