Idriss Elba atunukiwa hadhi: Sasa ni ‘Sir Idris Elba’

UINGEREZA: MUIGIZAJI nyota wa kimataifa, Idris Elba, ameandika ukurasa mpya katika maisha yake baada ya kutunukiwa rasmi hadhi ya ‘Sir’ na Mfalme Charles III wa Uingereza kutokana na mchango wake mkubwa katika kuwasaidia vijana.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 53, ambaye amewahi kung’ara kupitia tamthilia maarufu za ‘The Wire na Luther’, alipokea heshima hiyo katika hafla maalum iliyofanyika ndani ya Kasri la Windsor mbele ya Mfalme Charles III.
Katika tukio hilo la kihistoria, mfalme alifuata utamaduni wa kifalme wa karne nyingi kwa kugusa mabega ya Idris Elba kwa upanga maalum huku akiwa amepiga goti, hatua iliyomfanya rasmi kuitwa ‘Sir Idris Elba’.
Baada ya hafla hiyo, Sir Idris hakuficha furaha yake na aliwaambia mashabiki wake kupitia mitandao ya kijamii. Akiwa pamoja na mke wake, Sabrina Elba, akisema, “Tunashukuru. Kazi inaendelea.”
Idris Elba alitunukiwa heshima hiyo kutokana na kazi kubwa anayofanya kupitia taasisi ya Elba Hope Foundation aliyoianzisha pamoja na Sabrina mwaka 2022. Taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele kusaidia vijana kupata elimu, kupambana na ukosefu wa ajira pamoja na kusaidia jamii zinazokabiliwa na changamoto za chakula.
Hata hivyo, Sir Idris hakuwa mtu pekee aliyeng’ara katika hafla hiyo. Mastaa wa mchezo wa skating wa Olimpiki, Jayne Torvill na Christopher Dean, pia walitunukiwa heshima za kifalme, huku mwigizaji na mchekeshaji maarufu Meera Syal naye akitunukiwa hadhi ya ‘Dame’ kutokana na mchango wake katika sanaa na shughuli za kijamii.




