Kwingineko

Waargentina wawili wakiri kutoa rushwa katika kashfa ya ufisadi FIFA

NEW YORK: WATENDAJI wawili wa kampuni ya masoko ya michezo kutoka Argentina, Hugo Jinkis na mwanawe Mariano Jinkis, wamekiri kutoa rushwa kwa maofisa wa soka duniani ili kupata haki za matangazo ya mashindano mbalimbali yenye thamani kubwa.

Wawili hao, ambao ni baba na mwana, walikiri makosa hayo Alhamisi katika makubaliano na waendesha mashtaka nchini Marekani yaliyowezesha kuepuka kufikishwa mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa kesi.

Jinkis na Mariano walikuwa miongoni mwa watu walioshtakiwa kufuatia uchunguzi mkubwa wa rushwa uliotikisa Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) mwaka 2015, pamoja na mashirikisho ya soka ya Amerika Kusini na Amerika Kaskazini.

Uchunguzi huo ulioongozwa na mamlaka za Marekani ulihusisha pia misako katika ofisi za maofisa wa FIFA mjini Zurich, Uswisi, na kusababisha mfululizo wa kukamatwa, kufunguliwa mashtaka, hukumu na kukiri makosa kwa watuhumiwa mbalimbali.

Katika makubaliano yao na waendesha mashtaka, wawili hao pia wamekubali kunyang’anywa dola milioni 50 za Marekani, ikiwa ni sehemu ya adhabu iliyokubaliwa.
Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, Jinkis na mwanawe walikiri kwamba walitoa makumi ya mamilioni ya dola kama rushwa kwa viongozi wa soka ili kupata uungwaji mkono katika jitihada zao za kunyakua haki za matangazo na masoko ya mashindano mbalimbali ya soka.

Wawili hao ni wamiliki wenza wa kampuni ya masoko ya michezo ya Argentina, Full Play, ambayo ilihusika katika mikataba ya haki za matangazo ya mashindano mbalimbali.

Nyaraka za mahakama zinaeleza kuwa rushwa hizo zilitumika kusaidia kampuni hiyo kupata haki za kibiashara za matangazo ya michezo ikiwemo mechi za kufuzu Kombe la Dunia na Copa América.

Kesi hiyo ni sehemu ya sakata kubwa la rushwa lililoibuliwa mwaka 2015 na ambalo lilisababisha mabadiliko makubwa ndani ya FIFA na mashirikisho yake, huku viongozi kadhaa wa soka duniani wakikabiliwa na mashtaka nchini Marekani.

Makubaliano ya Jinkis na waendesha mashtaka yanaashiria hatua nyingine muhimu katika uchunguzi huo uliodumu kwa zaidi ya muongo mmoja.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button