Vigogo kukutana mapema Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2026/27

MONACO: DROO ya hatua ya ligi ya michuano ya UEFA Champions League msimu wa 2026/27 imezua hamasa kubwa baada ya vigogo wa soka la Ulaya kukutana katika mechi zinazotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Droo hiyo iliyofanyika Monaco imepangwa kwa mfumo mpya wa hatua ya ligi, ambapo kila timu itacheza jumla ya mechi nane, nne nyumbani na nne ugenini, dhidi ya wapinzani tofauti.
Miongoni mwa michezo inayosubiriwa kwa hamu ni Manchester City dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG) pamoja na Manchester City dhidi ya Barcelona, huku PSG pia ikitarajiwa kukutana na Barcelona.
Kwa upande mwingine, Arsenal imepangwa michezo migumu dhidi ya Real Madrid na Bayern Munich, hali inayofanya safari yake katika hatua ya ligi kuwa moja ya zinazofuatiliwa zaidi.
Liverpool nayo imepangwa kukutana na Atlético Madrid na Inter Milan, huku Manchester United ikikabiliwa na mtihani dhidi ya Bayern Munich na Atlético Madrid.
PSG, ambayo ni mabingwa watetezi wa Champions League, itakuwa na kazi kubwa ya kutetea taji lake baada ya kupangwa dhidi ya Barcelona na Manchester City katika hatua hii.
Hatua ya ligi itaanza Septemba 8, 2026, huku mechi za mwisho za hatua hiyo zikitarajiwa kuchezwa Januari 27, 2027.
Timu nane zitakazomaliza katika nafasi za juu zitaingia moja kwa moja hatua ya 16 bora, wakati timu zitakazomaliza nafasi ya tisa hadi 24 zitacheza play-off kuwania nafasi ya kuingia hatua hiyo.
Fainali ya Champions League 2026/27 imepangwa kufanyika Juni 5, 2027, katika Uwanja wa Metropolitano jijini Madrid, Hispania.




