Tulia Ackson: viongozi wapewe nafasi kuinua Soka la Wanawake

DODOMA: SPIKA Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya TFF, Dk Tulia Ackson, amesema mpango mkakati wa soka la wanawake ni hatua muhimu katika kuhakikisha mchezo huo unakua na kufikia viwango vya juu.
Akifungua warsha ya siku tatu ya kuwajengea uwezo wasimamizi na viongozi wa soka la wanawake, inayoendeshwa na FIFA na kuandaliwa na TFF, Dk Tulia amesema mafanikio ya wachezaji wa kike tayari yameifanya Tanzania kutambulika kwa kuwa na vipaji bora, hivyo viongozi wana wajibu wa kuweka mazingira yatakayowawezesha kufika mbali zaidi.
Amesema pamoja na changamoto zilizopo, Tanzania ipo katika hatua nzuri ya kusonga mbele, huku akisisitiza kuwa Bodi ya Wadhamini ya TFF iko tayari kushirikiana na viongozi na wadau kuhakikisha soka la wanawake linaendelea kupiga hatua.
Dk Tulia amewataka waliopewa dhamana ya kusimamia na kuendeleza soka la wanawake kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, kuwapa moyo wachezaji na kutowakatisha tamaa wale wanaohitaji msaada wa kiufundi na kiuongozi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa viongozi kuwa mfano bora kwa jamii na kuweka mifumo itakayowezesha Tanzania kupata wachezaji wengi wenye uwezo, ili soka la wanawake nalo lipewe kipaumbele na kufikia hadhi inayostahili.
“Tunataka kuwaona wachezaji wetu wakifika mbali zaidi na kuitangaza Tanzania kupitia vipaji vyao.”
Akizungumzia mchango wa Serikali, Dk Tulia amesema Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, ameendelea kutoa kipaumbele kwa maendeleo ya soka la wanawake pamoja na timu za vijana, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kujenga kizazi kipya cha wachezaji watakaoiwakilisha Tanzania kwa mafanikio.
Warsha hiyo ya siku tatu inalenga kuongeza maarifa na uwezo wa viongozi na wasimamizi katika kuendesha na kuendeleza soka la wanawake kwa mtazamo wa kimkakati na endelevu.




