Kwingineko

Casemiro atua Inter Miami, MLS wamchunguza

MIAMI: Klabu ya Inter Miami imetangaza rasmi kumsajili kiungo mkongwe wa Brazil, Casemiro, lakini muda mfupi baada ya kutangaza usajili huo, Ligi Kuu ya Soka ya Marekani (MLS) imefungua uchunguzi kuhusu madai ya ukiukwaji wa kanuni za usajili (tampering) zinazohusiana na dili hilo.

Casemiro mwenye umri wa miaka 34 anajiunga na Inter Miami kama mchezaji huru baada ya kutoongeza mkataba katika klabu Manchester United kufuatia kumalizika kwa kipindi chake cha miaka minne katika klabu hiyo.

Nyota huyo mwenye mechi 91 akiwa na timu ya taifa ya Brazil pia amewahi kutwaa mataji matano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Real Madrid.

Akiwasili Miami, Casemiro atakuwa sehemu ya kikosi chenye nyota wakubwa duniani akiwemo Lionel Messi, Rodrigo De Paul, huku klabu hiyo ikimilikiwa kwa pamoja na nguli wa soka England, David Beckham.

Mmiliki mkuu wa Inter Miami, Jorge Mas, alisema usajili wa Casemiro unaonesha dhamira ya klabu hiyo kuendelea kujenga kikosi chenye ushindani wa hali ya juu.

“Kuja kwa Casemiro kunaakisi maono na malengo ya Inter Miami. Haturidhiki kamwe, tunaendelea kukua, kuboresha kikosi na kuinua viwango vyetu kila msimu,” alisema Mas.

Hata hivyo, MLS imetangaza kuchunguza madai ya Inter Miami kuvunja taratibu za ligi katika mchakato wa usajili huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya ligi hiyo, uchunguzi unaendelea huku taarifa zote muhimu zikikusanywa kabla ya hatua yoyote kuchukuliwa.
MLS pia imeeleza kuwa makubaliano kati ya Inter Miami na LA Galaxy kuhusu haki ya usajili wa Casemiro yatatangazwa baada ya uchunguzi huo kukamilika.

Usajili wa Casemiro unaifanya Inter Miami kuendelea kuwa klabu yenye mkusanyiko mkubwa wa mastaa ndani ya MLS, baada ya hivi karibuni pia kuimarisha kikosi chake kwa nyota mbalimbali wa kimataifa. Klabu hiyo ilitwaa taji lake la kwanza la MLS Cup mwezi Desemba mwaka jana na mwezi Aprili ilihamia rasmi katika uwanja wake mpya.

Hata hivyo, si mara ya kwanza Inter Miami kukumbwa na changamoto zinazohusiana na usajili. Mwaka 2020 klabu hiyo ilitozwa faini ya dola milioni mbili za Marekani baada ya uchunguzi wa MLS kubaini ilikiuka kanuni za matumizi ya mishahara kufuatia usajili wa kiungo wa Ufaransa, Blaise Matuidi, kutoka Juventus.

Kwa upande wake, Casemiro amesema amevutiwa na mradi wa Inter Miami na anaamini bado ana mengi ya kushinda katika maisha yake ya soka.

“Mradi ambao klabu imenionyesha pamoja na juhudi walizofanya kunileta hapa umenigusa sana. Nimekuja kushinda na kuendelea kukua,” alisema kiungo huyo.

Naye David Beckham amesema ana furaha kubwa kumuona mshindi huyo wa mataji mengi akichagua Miami kuwa hatua inayofuata katika maisha yake ya soka.

“Casemiro ni mshindi wa kweli. Baada ya mafanikio makubwa akiwa Real Madrid na Manchester United, ninafurahi ameamua kuifanya Miami kuwa nyumbani kwake jipya,” alisema Beckham.

Related Articles

Back to top button