Vieira atwikwa Genoa

KIUNGO wa zamani wa Arsenal na timu ya taifa ya Ufaransa Patrick Vieira ametangazwa kuwa kocha mpya wa klabu iliyo kwenye hatari ya kushuka daraja kwenye msimamo wa Serie A ya Genoa CFC.
Vieira mwenye miaka 48 anachukua mikoba ya Alberto Gilardino aliyefutwa kazi Jumanne wiki hii akiiacha klabu hiyo katika nafasi ya 17 pointi moja juu ya Lecce, Monza na Venezia walio kwenye mstari wa kushuka daraja baada ya timu zote hizo kucheza michezo 12.
“Genoa CFC inatangaza kwamba Patrick Vieira amekabidhiwa rasmi majukumu ya kiufundi ya kikosi chetu cha kwanza. Kocha mpya ataongoza mazoezi ya kwanza leo mchana baada ya kusaini kandarasi katika ofisi zetu makao makuu za Villa Rostan.” – klabu ilisema katika taarifa yake.
Vieira aliyeshinda kombe la dunia la FIFA mwaka 1998 akiwa na Ufaransa alianza career yake ya ukocha katika timu za New York City, Nice, Crystal Palace na kazi ya mwisho akiwa na Strasbourg inayoshika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligue 1 ambako mkataba wake ulisitishwa kwa makubaliano ya pande mbili.