Ligi Ya Wanawake

‘Ukizitoa Simba, Yanga wengine tunajipigia tu’

KLABU ya Soka ya Wanawake, Ceasiaa Queens imesema timu wanazozihofia ni wakubwa watatu yaani JKT Queens, Simba Queens na Yanga Princess lakini wengine wote wanajipigia tu.

Akizungumza na SpotiLeo Kocha Msaidizi wa Ceasiaa Aziz Gubwe amesema timu hizo wanazihofia kutokana na ubora wa vikosi vyao na wanatarajia kupata ushindani mkali pindi watakapokutana.

Amesema kitu kingine timu hizo zina wachezaji wengi wenye uzoefu tofauti na wao ndio kwanza wanajijenga ili kuwa timu tishio kwa siku zijazo.

“Kila timu ni nzuri lakini Simba na Yanga zina wachezaji wengi wa kimataifa na wenye uzoefu, ukicheza nazo ni lazima ujipange vizuri, ila haimaanishi sisi ni wabovu tumejipanga kupambana,”amesema.

Kocha huyo amesema wanataka kutumia muda wa wiki mbili za ligi kusimama kujitengeneza na kujiweka imara zaidi na kuhakikisha wanatimiza malengo kama sio kuchukua ubingwa basi angalau hadi kufika mwisho wa msimu wanamaliza kwenye nne bora.

Ligi ya mpira wa miguu ya wanawake imesimama kupisha kalenda ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kwa timu ya taifa ya wanawake ya Twiga Stars kujiandaa na michezo ya kimataifa.

Gubwe amesema ndani ya wiki hizo mbili wanaweza kurudi na kuwa tishio kwa kuwa kuna wachezaji wao wawili wa kimataifa waliochelewa kujiunga na timu watakuwa wamesharudi kujiandaa na michezo inayofuata.

Timu hiyo iko katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Wanawake baada ya kucheza michezo miwili na kati ya hiyo, imeshinda mmoja na kupoteza mmoja ikiwa na pointi tatu.

Related Articles

Back to top button