TETESI ZA USAJILI ULAYA
Man United haijamkatia tamaa De Jong
KOCHA wa klabu ya Manchester United Erik ten Hag amenuia kurudisha mashambulizi upya ya kumsajili kiungo wa Barcelona, Frenkie De Jong. Kwa muda mrefu tangu mwaka 2022, United imekuwa ikitupa ndoano kwa mchezaji huyo ambaye alikataa kuondoka Barcelona na hivyo kuzima ndoto za mashetani wekundu za kutaka kumsajili.
Ten Hag amekuwa muumini mkubwa wa kusajili wachezaji aliowahi kufanya nao kazi huko nyuma kama Anthony, De Ligt, Onana, Mazraoui na Martinez na sasa ameutaka uongozi wa klabu hiyo kujaribu tena kumsajili Frenkie De Jong ambaye kama waliotajwa hapo juu, aliwahi kumfundisha Ajax nchini Uholanzi.
De Jong aliyerejea kwenye kikosi mwezi huu baada ya majeraha ya kifundo cha mguu, aliwahi kusema kwamba hana mpango wa kuondoka Barcelona mpaka mkataba wake utakapokwisha mwaka 2026. Licha ya hivyo, United watarusha ndoano zao kwa mchezaji huyo katika dirisha lijalo la usajili la Januari.
Florian Wirtz kwenye rada za PSG
PARIS SAINT-GERMAIN wameandaa kiasi kikubwa cha pesa kukamilisha uhamisho wa staa wa Bayer Leverkusen, Florian Wirtz. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani anawindwa pia na klabu kubwa kama Liverpool na Manchester United.
Uwezo anaouonesha Wirtz umeivutia PSG ambapo taarifa zinaeleza kwamba klabu hiyo imeandaa dau la euro milioni 150 ili kuishawishi Leverkusen kumuachia mchezaji huyo. Kutokana na dau hilo kubwa, tayari PSG imekuwa kinara katika mbio hizo kwani si rahisi kwa klabu ya Liverpool na Man United kutoa pesa zinazokaribia dau hilo. Kwa msimu huu, Wirtz amecheza michezo 11 na kufunga mabao 6 pamoja na pasi 1 ya bao.
Newcastle kumuachia Trippier
MCHEZAJI wa kimataifa wa England na timu ya Newcastle, Kierran Tripper ametajwa kukaribia kuondoka klabuni hapo kutokana na kukosa nafasi katika kikosi hicho kinachonolewa na Eddie Howe. Newacatle inakaribisha ofa kwa mchezaji huyo ambaye ni mmoja ya wachezaji wanaolipwa mshahara mkubwa kikosini, akipokea pauni 120,000 kwa wiki.
Kwa kiwango hicho kikubwa cha mshahara na dakika chache tu anazotumika uwanjani, ni wazi kwamba Trippier atatimka katika madirisha ya usajili yanayofuata na tayari imeelezwa kwamba kuna baadhi ya klabu kutoka Saudi Arabia zinamtaka, ni suala la Newactle kusubiri ofa itakayowaridhisha ili kumuachia.
Kyle Walker kufuata pesa Urabuni
NAHODHA wa Manchester City, Kyle Walker anawindwa na klabu ya Al- Ahli ya nchini Saudi Arabia. Mlinzi huyo mwenye umri wa miaka 34 ana mkataba na City hadi mwaka 2026 na inavyoonekana hakuna dalili zozote za kumuongezea mkataba mchezaji huyo.
Taarifa zinaeleza kwamba endapo dili hilo litakamilika, Walker atakuwa mmoja ya wachezaji wa kiingereza wanaolipwa mshahara mkubwa kwani Ali- Ahli ipo tayari kumpa mshahara wa dola 400, 000 kwa wiki, zaidi ya mara mbili ya anaoupokea akiwa City.
Klabu hiyo ya Saudi inamtaka mchezaji huyo mwenye uzoefu mkubwa na Ligi Kuu Engand ambapo alijiunga na Man City mwaka 2017 na ameichezea klabu hiyo michezo 308, akifunga mabao 6 na kutoa pasi 23 za mabao kwenye mashindano yote. City itakuwa tayari kumuachia bingwa huyo wa EPL mara 6 kwa ada ya pauni milioni 15 tu katika dirisha la usajili la kiangazi.
Chelsea kumtoa Chilwell kwa mkopo
KLABU ya Chelsea imedhamiria kumtoa mlinzi wake wa kushoto Ben Chilwell kwa mkopo wa muda mrefu katika dirisha dogo la usajili la Januari. Kocha mkuu wa kikosi hicho aliweka wazi kuwa klabu ilikuwa tayari kumuuza Chilwell pamoja na wachezaji wengine katika dirisha la usajili lililopita lakini hawakufanikiwa.
Kwa kukosa kabisa nafasi katika kikosi cha kwanza cha ‘The Blues’, ni wazi kwamba Chilwell ataondoka klabuni hapo na taarifa zinaeleza kwamba Chelsea ipo tayari kumuachia mchezaji huyo kwa mkopo wa muda mrefu, mkopo wa takribani miezi 18. Chilwell amecheza dakika 45 tu za kombe la Carabao dhidi ya Barrow, lakini bahati nzuri kwake ni kwamba klabu nyingi zitahitaji huduma yake pindi akiwekwa sokoni.
West Ham, Brentford na Fulham zinataka saini ya mchezaji huyo kumbakiza London lakini klabu za nje ya England pia zinamtaka kama vile Napoli na Marseille.
Dusan Vlahovic awindwa na Arsenal
WASHIKA mitutu wa London Arsenal wanamtupia jicho la karibu straika wa timu ya Juventus, Dusan Vlahovic ili kwenda kuongeza makali katika kikosi hicho kinachonolewa na Mikel Arteta.
Arsenal imeona mwanya huo baada ya taarifa kueleza kwamba Vlahovic ameshindwa kufikia hatma ya mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya na kibibi kizee cha Turin. Vahlovic ameingia kwenye orodha ya mastraika ambao Arsenal inawataka wakiwemo Viktor Gyokeres, Alexander Isak, Jonathan David na Marcus Thuram. Mkataba wake na Juventus unakwisha 2026 na Arsenal wana matumaini ya kumpata mshambuliaji huyo mserbia endapo bado hatakuwa amekubali kuongeza mkataba mpya na Juventus ifikapo majira ya kiangazi mwakani